MASOMO YA MISA, JULAI 17, 2022
DOMINIKA YA 16 YA MWAKA C
SOMO 1
Mwa. 18 : l-10
Bwana alimtokea Ibrahimu karibu na mialoni ya Mamre,
alipokuwa ameketi mlangoni pa hema yake mchana wakati wa hari. Akainua macho
yake akaona, na tazama, watu watatu wamesimama mbele yake. Naye alipowaona
alipiga mbio kuwalaki kutoka mlangoni pa hema, akainama mpaka nchi, akasema,
Bwana wangu, kama nimeona fadhili machoni pako nakuomba usinipite sasa mimi
mtumwa wako. Na yaletwe basi maji kidogo mkanawe miguu, mkapumzike chini ya mti
huu. Nami nitaleta chakula kidogo, mkaburudishe moyo, baadaye mwendelee, iwapo
mmemjia mtumwa wenu. Wakasema, Haya, fanya kama ulivyosema. Basi Ibrahimu
akaenda hima hemani kwa Sara, akasema, Himiza vipimo vitatu vya unga safi,
uukande, ufanye mikate. Ibrahimu akapiga mbio kwenda kundini, akaleta ndama wa
ng’ombe aliye laini, mzuri, akampa mtumishi, naye akahimiza kuiandaa. Akatwaa
siagi na maziwa, na ndama aliyoiandaa, akawaandikia mbele yao, akasimama karibu
nao chini ya mti, nao wakala. Wakamwambia, Yu wapi Sara mkeo? Akasema, Yumo
hemani. Akamwambia, Hakika nitakurudia wakati uu huu mwakani. na tazama, Sara
mkeo atapata mwana wa kiume.
Neno la Mungu...Tumshukuru Mungu
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 15 (K) 1
(K) Bwana, ni nani atakayekaa katika hema yako
Bwana, ni nani atakayefanya maskani yake
Katika kilima chako kitakatifu?
Ni yeye aendaye kwa ukamilifu,
Na kutenda haki;
Asemaye kweli kwa moyo wake,
Asiyesingizia kwa ulimi wake. (K)
Yeye ambaye hakumtenda mwenziwe mabaya,
Wala hakumsengenya jirani yake.
Machoni pake mtu asiyefaa hudharauliwa,
Bali huwaheshimu wamchao Bwana. (K)
Yeye ambaye hakutoa fedha yake apate kula riba,
Hakutwaa rushwa amwangamize asiye na hatia.
Mtu atendaye mambo hayo
Hataondoshwa milele. (K)
SOMO 2
Kol 1 :24-28
Nayafurahia mateso niliyo nayo kwa ajili yenu; tena
nayatimiliza katika mwili wangu yale yaliyopungua ya mateso ya Kristo, kwa
ajili ya mwili wake, yaani, kanisa lake, ambalo nimefanywa mhudumu wake,
sawasawa na uwakili wa Mungu, niliopewa kwa faida yenu, nilitimize neno la
Mungu; siri ile iliyofichwa tangu zamani zote na tangu vizazi vyote, bali sasa
imefunuliwa kwa watakatifu wake; ambao Mungu alipenda kuwajulisha jinsi ulivyo
utajiri wa utukufu wa siri hii katika Mataifa, nao ni Kristo ndani yenu; tumaini
la utukufu; ambaye sisi tunamhubiri habari zake, tukimwonya kila mtu, na
kumfundisha kila mtu katika hekima yote, tupate kumleta kila mtu mtimilifu
katika Kristo.
Neno la Mungu...Tumshukuru Mungu
SHANGILIO
Yn. 14 :23
Aleluya, aleluya, Mtu akinipenda, atalishika neno langu;
Na Baba yangu atampenda; Nasi tutakuja kwake. Aleluya.
INJILI
Lk. 10 :38-42
Ikawa katika kuenenda kwao Yesu aliingia katika kijiji
kimoja; mwanamke mmoja jina lake Martha akamkaribisha nyumbani kwake. Naye
alikuwa na umbu lake aitwaye Mariamu, aliyeketi miguuni pake Yesu, akasikiliza
maneno yake. Lakini Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi; akamwendea,
akasema, Bwana, huoni vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke
yangu? Basi mwambie anisaidie. Bwana akajibu akamwambia, Martha, Martha,
unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi; lakini kinatakiwa kitu kimoja
tu; na Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa.
Neno la Bwana...Sifa kwako, ee Kristo
Copyright © 2022 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment