“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya Kwaresima
APRILI 4, 2022
JUMATATU, JUMA LA 5 LA KWARESIMA
SOMO 1 Dan.13:41-62
INJILI Yn. 8:12-20
Karibuni
ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana
katika Zaburi yetu ya wimbo wa katikati tunakutana na ujumbe-Bwana ndiye
mchungaji mwema sintapungukiwa na kitu. Haya ni maneno ya Zaburi ya 23. Mzaburi
anashuhudia tumaini lake kwa Mungu kama mchungaji. Wanyama kama kondoo ni
wanyama dhaifu mbele ya wanyama kama simba na chui. Bila uwepo wa mchungaji
mahiri, wanyama kama hawa huraruliwa kwa haraka mbele ya simba.
Bila
mchungaji mahiri, wanyama kama hawa hawataweza kula majani;-watanyanyaswa tu.
Ni tofauti na wanyama jeuri kama simba au chui na fisi.
Katika
somo la kwanza, tunagundua kwamba kati ya wanadamu, wapo ambao ni kama kondoo
na wengine ni wajeuri. Kondoo hawana nguvu au mabavu kama Susana anavyoonekana
katika somo la kwanza. Wale wazee wanaomhukumu Suzana tunawafananisha na
wanyama kama Simba. Hawa wanakuja kwa lengo la kurarua kila wakati. Hawa
huwainulia wengine mabaya, huwaonea watu, hutumia nguvu zao kuwafaidi kondoo.
Katkai
ulimwengu tutakutana na watu kama hawa. Yesu alikutana na viongozi wa Kiyahudi
waliompeleka kama kondoo asiyekuwa na hatia, wakampiga bila huruma. Sisi
tunapaswa kumweka Mungu kuwa kinga yetu. ulimwenguni tutakumbana na watu kama
hawa. Wapo baadhi yetu ambao kuishi nao au kufanya nao kazi ni kugumu zaidi
kuliko kukutana na simba.
Tumtegemee
Mungu. Tunapaswa kumwita Mungu kila wakati. Katika kipindi chetu cha kwaresima,
ni kipindi cha kumuita Mwenyezi Mungu. Atuepushe na maadui wetu. Wapo
wanaotutakia mabaya. Lakini kwa nguvu ya Mungu tutawashinda. Mungu atatuinulia
watu kama akina Danieli ambao watakuja na kututetea.
Yesu
anasema katika injili ya leo kwamba yeye ni Nuru ya ulimwengu. Na yeyote
amfuataye, hatakuwa akitembea gizani bali atakuwa na uzima wa milele. Twende
kwa Yesu tupate Mwanga. Wengi wetu katika ulimwengu, bado tunaishi katika giza,
bado tunafuata mikumbo ya wadhambi, kama umati wa leo katika somo la kwanza
uliotaka kumteketeza Suzana.
Danieli
alipata mwanga toka kwa Mungu. Itakuwaje kama sisi sote tutaomba na kupata
Mwanga toka kwa Yesu ili tuweze kutoa hukumu zenye kufaa? Wengi katika jamii
wamepakwa matope kutokana na ukosefu wa watu kama kina Daniel. Wengi wamepoteza
kazi zao au kushindwa kesi au hata kupoteza maisha kutokana na kufuata
wasemacho umati/mob. Tuwe makini kuchambua kile kiamuliwacho na umati. Bwana
Yesu atupe Mwanga wa kufanya maamuzi ya namna hii.
Copyright ©2013-2022 ©FurKat,
Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment