MASOMO YA MISA, APRILI 4, 2022
JUMATATU, JUMA LA 5 LA KWARESIMA
SOMO 1
Dan.13:41-62
Palikuwa na mtu mmoja jina lake
Yoakimu, akikaa Babeli, naye ameoa mke jina lake Susana binti Helkia, mwanamke
mzuri sana na mcha Mungu. Wazee wake nao walikuwa wenye haki, pia wamemfundisha
binti yao sawasawa na Torati ya Musa. Basi Yoakimu alikuwa mwungwana tajiri, na
karibu na nyumba yake alikuwa na bustani nzuri; hivyo Wayahudi humwendea, maana
alikuwa ni mwenye heshima kupita wengineo wote. Mwaka ule ule wakaamriwa wawili
miongoni mwa wazee wa watu ili kuamua, watu wa namna ile ambao Bwana aliwanena,
ya kama ufisadi ulitoka Babeli kwa wazee waamuzi waliohesabiwa kuwa wanatawala
watu. Hao walikuwa wakienda mara nyingi kuzuru kwenye nyumba yake Yoakimu; na
wote wenye mashtaka yoyote desturi yao wakawajia huko. Basi watu walipoondoka
kwenda zao panapo saa sita, Susana huingia katika bustani ya mumewe ili
kutembea. Nao wale wazee humwona kila siku anakwenda kutembea; hata wakawaka
tamaa kwa sababu yake. Ndipo walipozipotosha nia zao, wakayageuza upande macho
yao wasiweze kutazama mbinguni wala kukumbuka hukumu za haki. Ikawa walipongoja
wakati wa kufaa, yeye aliingia bustanini kama ilivyokuwa desturi yake pamoja na
wajakazi wawili, naye alitaka kuoga kwa sababu kulikuwa na joto. Wala hapakuwa
na mtu yeyote isipokuwa wale wazee wawili, ambao wamejificha wakimvizia. Basi
akawaambia wajakazi wake, Nileteeni mafuta na sabuni, mkaifunge milango ya
bustani ili nioge . Mara wale wajakazi walipokwishas kutoka, wale wazee wawili
waliondoka wakamwendea mbio, wakasema, Tazama, milango ya bustani imefungwa
asiweze kutuona mtu yeyote nasi tunakupenda sana; haya! Basi, utukubali na
ulale nasi. La! Hutaki tutakushuhudia ya kuwa hapa palikuwapo na kijana pamoja
nawe, ndiyo sababu uliwaruhusu wajakazi wako. Basi Susana aliugua akasema,
Nimesongwa pande zote, maana nikilitenda hilo ni mauti yangu; nisipolitenda
siwezi kuokoka mikononi mwenu. Ni afadhali niangukie katika mikono yenu na
kukataa, kuliko kutenda dhambi machoni pa Mungu. Mara Susana akapiga kelele kwa
sauti kuu; nao wale wazee wawili wakampigia kelele pia. Kisha mmoja wao akakimbia,
akaifungua milango ya bustani. Hivyo watumishi wa nyumbani waliposikia kelele
bustanini, wao waliingia kwa kasi kwa mlango wa nyuma ili waone ni nini
iliyompata. Lakini wale wazee waliisimulia hadith yao nao watumishi wakaona
aibu kabisa, kwa maana Susana hakuchongelewa habari ya namna hiyo wakati
wowote.
Ikawa kesho yake watu
walipokusanyika kwa Yoakimu mumewe, wale wazee wawili wakaja nao, wamejaa
kusudi lao ovu juu ya Susana la kumfisha. Wakasema mbele ya watu, "Mwiteni
Susana binti Helkia, mkewe Yoakim, aje hapa". Basi akaenda kuitwa; naye
akaja pamoja na baba yake na mama yake, na watoto wake, na jamaa zake wote.
Naye huyo Susana alikuwa mwanamke mwenye adabu, mzuri wa uso; basi hao watu
wabaya waliamuru afunuliwe uso, maana alifunikwa utaji, ili washibe uzuri wake.
Kwa hiyo rafiki zake na wote waliomtazama wakasikitika. Ndipo wale wazee wawili
waliposimama katikati ya watu, wakaweka mikono yao juu ya kichwa chake. Naye
akatoka machozi, akatazama juu mbinguni, kwa maana moyo wake ulimtumaini Mungu.
Wale wazee wakasema, Sisi tulipokuwa tukitembea bustanini peke yetu, huyu
aliingia pamoja na wajakazi wawili, wakaifunga milango ya bustani, naye mara
akawaruhusu wajakazi. Kisha kukatokea kijana, ambaye amejificha humo,
akamwendea akalala naye. Walakini sisi tungaliko pembeni mwa bustani, tuliona
ubaya huo, tukamwendea mbio. Hata tukiwa tumewaona pamoja, yule kijana
hatukuweza kumkamata, maana alikuwa mwenye nguvu kuliko sisi, akifungua milango
akaepuka. Bali huyu tulimkamata, tukauliza yule kijana yu nani, asikubali
kutuambia. Hayo basi, tunashuhudu. Basi waliohudhuria wakawasadiki, wakiwa
wazee wa watu na waamuzi; hivyo wakahukumu auawe. Mara Susana akalia kwa sauti
kuu, akasema, Ee Mungu wa milele, Wewe wajua yaliyositirika, wajua mambo yote
yasijekuwako, Wewe wajua ya kwamba wananishuhudia uongo, na tazama, imenipasa
kufa; walakini sikufanya mambo kama hayo, ambayo watu hawa wameyabuni juu yangu
kwa ukorofi.
Naye Bwana akaisikia sauti yake.
Kwa hiyo, alipochukuliwa huyo kwenda kuuawa, Mungu alimchocheleza roho kijana
mmoja, jina lake Danieli; naye akapaza sauti akasema, Mimi simo; mimi sina
hatia kwa habari ya damu yake mwanamke huyu. Mara wote wakamgeukia, wakasema,
Maneno hayo uyasemayo, maana yake nini? Akasimama katikati, akasema, Enyi bani
Israeli, mmekuwa wapumbavu, hata kumhukumu binti Israeli bila kuhoji wala
kupata hakika ya kweli? Rudini hukumuni; mradi hao wanamshuhudia uongo.
Basi watu wote walirejea kwa
haraka, nao wale wazee wakamwambia, Njoo uketi kati yetu, utujulishe habari
hiyo, endapo Mungu amekupa wewe heshima yam zee. Hapo Danieli aliwaambia, Watu
hawa wawili watengwe, nami nitawahoji. Basi wakiisha kutengwa, akamwita mmoja
wao akamwambia, Ewe uliyepata kuwa mzee katika uovu, sasa dhambi zako
zimekukalia, ulizozitenda zamani kwa kuhukumu isivyo haki, kumpatiliza asiye na
hatia na kumwachilia mwovu; lakini Bwana asema, Asiye na hatia, mwenye haki,
usimwue. Haya! Basi, wewe ulimwona kwa macho; useme; Chini ya mti gani
ulipowaona wakikaa pamoja? Naye akajibu, Chini ya msandarusi. Danieli akasema,
Hakika umesema uongo juu ya kichwa chako mwenyewe; maana sas hivi malaika wa
Mungu amepokea hukumu ya Mungu, akukate vipande viwili. akamtenga huyo tena,
akaamuru kumleta yule mwingine, akamwambia, Ewe mzao wa Kanaani, wala si wa
Yuda, uzuri umekudanganya, na tamaa imeupotosha moyo wako. Hivyo ndivyo
ulivyowafanyia binti za Israeli, na kwa hofu walitembea nawe; bali huyu binti
Yuda hakuweza kuustahimili uovu wako. Haya! Basi, nawe useme; Chini ya mti gani
ulipowaona wakikaa pamoja? Naye akajibu, Chini ya mkwaju. Danieli akamwambia,
Hakika wewe nawe umesema uongo juu ya kichwa chako mwenyewe; maana malaika wa
Mungu yu tayari, anakungoja mwenye upanga, akukate vipande viwili; ili
awaangamize nyote wawili.
Mara hiyo makusanyiko yote wakapaza
sauti kwa nguvu, wakamhimidi Mungu awaokoaye wamtumainio. Wakawaondokea wale
wazee wawili, kwa maana Danieli ameuhakikisha ushuhuda wao wa uongo hata
vinywani mwao wenyewe. Wakawatenda kwa Torati ya Musa kama vile walivyokusudia
kwa ukorofi kumfanyia jirani yao; wakawaua; na mwenye damu isiyo na hatia
aliokolewa siku ile.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 23 (K) 4
(K) Nijapopita katika bonde la
uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami.
Bwana ndiye mchungaji wangu,
Sitapungukiwa na kitu.
Katika malisho ya majani mabichi
hunilaza,
Kando ya maji ya utulivu
huniongoza. (K)
Hunihuisha nafsi yangu; na
kuniongoza,
Katika njia za haki kwa ajili ya
jina lake.
Naam, nijapopita kati aya bonde la
uvuli wa mauti
Sitaogopa mabaya; kwa maana Wewe
upo pamoja nami,
Gongo lako na fimbo yako
vyanifariji. (K)
Waandaa meza mbele yangu,
Machoni pa watesi wangu.
Umenipaka mafuta kichwani pangu,
Na kikombe change kinafurika. (K)
Hakika wema na fadhili zinanifuata,
Siku zote za maisha yangu,
Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana
milele. (K)
SHANGILIO
Yn. 6:64, 69
Maneno yako, Ee Bwana, ni roho,
tena ni uzima, Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
INJILI
Yn. 8:12-20
Yesu aliwaambia tena akasema, Mimi
ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa
na nuru ya uzima.
Basi Mafarisayo wakamwambia, Wewe
unajishuhudia mwenyewe; ushuhuda wako si kweli.
Yesu akajibu, akawaambia, Mimi
ningawa ninajishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu ndio kweli; kwa sababu najua
nilikotoka na niendako; lakini ninyi hamjui nilikotoka wala niendako. Ninyi
mwahukumu kwa kufuata mambo ya mwili; mimi simhukumu mtu. Nami nijapohukumu,
hukumu yangu ni kweli; kwa kuwa mimi si peke yangu, bali ni mimi nay eye
aliyenipeleka. Tena katika torati yenu imeandikwa kwamba, Ushuhuda wa watu
wawili ni kweli. Mimi ndimi ninayejishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenipeleka
ananishuhudia.
Basi wakamwambia, Yuko wapi Baba
yako? Yesu akajibu, Mimi hamnijui, wala Baba yangu hammjui kama mngalinijijua
mimi, mngalimjua na Baba yangu.
Maneno hayo aliyasema alipokuwa
akifundisha hekaluni, katika chumba cha hazina; wala hakuna mtu aliyemkamata,
kwa sababu saa yake ilikuwa haijaja bado.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee
Kristo.
Copyright © 2022, "MASOMO YA
MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings
reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment