ASALI
ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari
ya kila siku
Alhamisi,
Februari 17, 2022,
Juma
la 6 la Mwaka wa Kanisa
Mk
8: 27-33.
UHURU
KUTOKA KATIKA HOFU YA MSALABA!
Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa tafakari ya neno la Bwana asubuhi ya
leo. Neno la Bwana katika Zaburi ya wimbo wa katikati linasisitizia juu ya
upendo alio nao mwenyezi Mungu kwa maskini. Kwa hakika Bwana huwasikiliza
maskini, mbele yake maskini wanayo hadhi kuu. Mbele ya Bwana maskini akilia
haonekani kuwa kama msumbufu bali husikilizwa katika huruma kuu.
Tabia hii ya kimungu ni tafauti na tabia inayooneshwa na baadhi ya
wakristo wa enzi za Yakobo na Yakobo anakemea udhaifu wa namna hii. Wakristo
wake walionekana kuwastahi zaidi matajiri kuliko maskini, cha ajabu kabisa ni
kwamba tabia hii iliingia hadi kanisani, kwamba tajiri alionekana kuwa mkristo
bora zaidi na wa maana kuliko maskini. Tajiri alipoingia kanisani, alionekana
kama roho mtakatifu ameingia ndani ya kanisa. Hivyo baadhi ya waaamini walianza
kumpatia heshima zaidi. Yakobo anakemea tabia za namna hii-kwanza kwa sababu
humfanya Mungu atambulike kama Mungu mbaguzi, mwenye kuwapenda matajiri na
kuwachukia maskini, pili, huwafanya wakristo watoe heshima zaidi kwa mwanadamu
zaidi kuliko Mungu kwani kila alipo tajiri au kiongozi mkubwa, heshima
huelekezwa zaidi kwake na hii humfanya Mungu asiabudiwe katika kina.
Neno hili litufundishe na sisi pia. Tusiwe na ubaguzi maishani mwetu
hasa makanisani mwetu. Kanisani ni mahali ambapo wote wanapaswa kusikilizwa,
hasa maskini na wagonjwa. Faraja yao ipo kanisani. Kanisa liwapatie faraja hii.
Kanisa liliundwa kwa nguvu na uwezo ya Roho Mtakatifu na sio kwa nguvu
ya fedha. Wakristo wengi wa mwanzo waliohusika katika kueneza injili wengi
walikuwa maskini na wagonjwa. Matajiri walikuwa wachache. Hata ikiwa kanisa
litakosa matajiri au likikosa majengo mazuri au wasomi wakubwa-bado litazidi
kuwepo na kuwa na nguvu kwani Roho ndiye afanyaye kazi ndani ya kanisa. Tuepuke
kuwastahi matajiri zaidi kuliko maskini.
Katika somo la injili, Bwana Yesu anawauliza wanafunzi wake juu ya
utambuzi wake yeye mwenyewe, kwamba watu hunena kwamba yeye ni nani? Petro
anatoa jibu zuri, na Yesu anafurahishwa na jibu hilo na pia anaendelea mbele
kumwelezea Petro juu ya utume na wajibu unaoambatana na cheo chake cha umasiha
kwamba itambidi ateswe na kuuawa kabla ya kufufuka.
Petro hakubaliani na mtazamo huu na hivyo anataka kumpinga Yesu na Yesu
anatumia maneno makali kabisa kumpinga Petro, anamwita Petro kuwa shetani, na
hivyo akae nyuma. Yesu alifanya jambo zuri, la kutafuta utambulisho wake toka
kwa wanafunzi wake na alifurahi kupata utambulisho wake toka kwa wanafunzi
wake.
Sisi nasi tunapaswa kuuliza juu ya utambulisho wetu katika eneo
tunaloishi-hii itatusaidia katika kujielewa zaidi. Wapo kati yetu ambao
hatujielewi na pia maisha yetu hayaeleweki. Tukishirikiana na wenzetu, tutaweza
kujitambua zaidi na kuwa watu bora zaidi.
Hivyo siku ya leo, mwulize mwenzako, je, mimi ni nani hapa? Maisha yangu
yakoje hapa? Ninatimiza wajibu wangu vipi? Majibu yao yaweza kuwa msaada mkubwa
sana kwetu. Pia tusisite kuwakemea tena kwa ukali wale wanaotutaka tubadili
mwenendo na msimamo wetu bora. Yesu alimkemea Petro kwa ukali. Nasi tuwakemee
marafiki wabaya, na wote walio na mawazo potofu yawezayo kuharibu maisha yetu.
Copyright
©2013-2022 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment