MASOMO YA MISA,
ALHAMISI Februari 17, 2022,
SOMO
Yak 2:1-9
Ndugu zangu, imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwe
nayo kwa kupendelea watu. Maana akiingia katika sinagogi lenu mtu mwenye pete
ya dhahabu na mavazi mazuri; kisha akiingia na maskini, mwenye mavazi mabovu;
nanyi mkimstahi yule aliyevaa mavazi mazuri, na kumwambia, Keti wewe hapa
mahali pazuri; na kumwambia yule maskini, Simama wewe pale, au keti miguuni
pangu, je! Hamkufanya hitilafu mioyoni mwenu, mkawa waamuzi wenye mawazo
mabovu? Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni, Je! Mungu hakuwachagua maskini wa
dunia wawe matajiri wa imani na warithi wa ufalme aliowaahidia wampendao? Bali
ninyi mmemvunjia heshima maskini. Je! Matajiri hawawaonei ninyi na kuwavuta
mbele ya viti vya hukumu? Hawalitukani jina lile zuri mliloitwa? Lakini
mkiitimiza ile sheria ya kifalme kama ilivyoandikwa, Mpende jirani yako kama
nafsi yako, mwatenda vema. Bali mkiwapendelea watu, mwafanya dhambi na
kuhukumiwa na sheria kuwa wakosaji.
Wimbo wa Katikati
Zab 34:1-6
Nitamhimidi Bwana kila wakati,
Sifa zake zi kinywani mwangu daima.
Katika Bwana nafsi yangu itajisifu,
Wanyenyekevu wasikie wakafurahi.
(K) Maskini huyu aliita, Bwana akasikia
Mtukuzeni Bwana pamoja nami,
Na tuliadhimishe jina lake pamoja.
Nalimtafuta Bwana akanijibu,
Akaniponya na hofu zangu zote.
(K) Maskini huyu aliita, Bwana akasikia
Wakamwelekea macho wakatiwa nuru,
Wala nyuso zao hazitaona haya.
Maskini huyu aliita, Bwana akasikia,
Akamwokoa na taabu zake zote.
(K) Maskini huyu aliita, Bwana akasikia
Somo la Injili
Mk 8:27-33
Siku ile Yesu alitoka na wanafunzi wake, wakaenda kwenye vijiji vya
Kaisaria-Filipi; na njiani akawauliza wanafunzi wake, akasema, Watu huninena
mimi kuwa ni nani? Wakamjibu, Yohana Mbatizaji; wengine, Eliya; wengine,
Mmojawapo wa manabii. Naye akawauliza, Na ninyi mnasema ya kuwa mimi ni nani?
Petro akamjibu, akamwambia, Wewe ndiwe Kristo. Akawaonya wasimwambie mtu habari
zake. Akaanza kuwafundisha kwamba imempasa Mwana wa Adamu kupatikana na mateso
mengi, na kukataliwa na wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa,
na baada ya siku tatu kufufuka. Naye alikuwa akinena neno hilo waziwazi. Petro
akamchukua, akaanza kumkemea. Akageuka, akawatazama wanafunzi wake, akamkemea
Petro, akasema, Nenda nyuma yangu, Shetani; maana huyawazi yaliyo ya Mungu,
bali ya wanadamu.
Neno la Bwana...sifa kwako ee Kristo
Copyright
© 2022, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora
– Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment