MASOMO YA MISA, JANUARI
7, 2022
IJUMAA BAADA YA
EPIFANIA
SOMO 1
1Yoh. 5:5-6, 8-13
Wapenzi: Mwenye
kuushinda ulimwengu ni nani, isipokuwa ni yeye aaminiye ya kwamba Yesu ni Mwana
wa Mungu? Huyu ndiye aliyekuja kwa maji wa damu, Yesu Kristo; si katika maji
tu, bali katika maji na katika damu. Kwamaana wako watatu washuhudiao
(mbinguni, Baba, na Neno, na Roho Mtakatifu, na watatu hawa ni umoja. Kisha
wako watatu washuhudiao duniani), Roho, na maji, na damu; na watatu hawa
hupatana kwa habari moja.
Tukiupokea ushuhuda wa
wanadamu, ushuhuda wa Mungu ni mkuu zaidi; kwa maana ushuhuda wa Mungu ndio
huu, kwamba amemshuhudia Mwanawe. Yeye amwaminiye Mwana wa Mungu anao huo
ushuhuda ndani yake. Asiyemwamini Mungu amemfanya kuwa mwongo, kwa kuwa
hakuuamini huo ushuhuda ambao Mungu amemshuhudia Mwanawe. Na huu ndio ushuhuda,
ya kwamba Mungu alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe. Yeye
aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima.
Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi
mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu.
Neno la Bwana…
Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 147:12-15, 19-20
(K) 12
(K) Msifu Bwana, Ee
Yerusalemu.
Msifu Bwana, Ee
Yerusalemu;
Msifu Mungu wako, Ee
Sayuni.
Maana ameyakaza mapingo
ya malango yako,
Amewabariki wanao ndani
yako. (K)
Ndiye afanyaye amani
mipakani mwako,
Akushibishaye kwa unono
wa ngano.
Huipeleka amri yake juu
ya nchi;
Neno lake lapiga mbio
sana. (K)
Humhubiri Yakobo neno
lake,
Na Israeli amri zake na
hukumu zake.
Hakulitendea taifa
lolote mambo kama hayo,
Wala hukumu zake
hawakuzijua. (K)
SHANGILIO
1Tim. 3:16
Aleluya, aleluya,
Sifa kwako, Ee Kristo,
uliyehubiriwa katika mataifa; Sifa kwako, Ee Kristo, aliyeaminiwa katika
ulimwengu.
Aleluya.
INJILI
Lk. 5:12-16
Ikawa Yesu alipokuwa
katika mmojawapo wa miji ile, tazama, palikuwa na mtu amejaa ukoma; naye
alipomwona Yesu alianguka kifudifudi, akamwomba akisema, Bwana, ukitaka, waweza
kunitakasa. Naye akaunyosha mkono wake, akamgusa akisema, Nataka; takasika. Na
mara ukoma wake ukamwondoka. Akamkataza asimwambie mtu, ila, Nenda ukajionyeshe
kwa kuhani; ukatoe kwa ajili ya kutakasika kwako kama Musa alivyoamuru, iwe
ushuhuda kwao.
Lakini habari zake
zikazidi kuenea, wakakutanika makutano mengi wamsikilize na kuponywa magonjwa
yao. Lakini yeye alikuwa akijiepua, akaenda mahali pasipokuwa na watu, akaomba.
Neno la Bwana… Sifa
kwako Ee Kristo.
-------------------------
Copyright
© 2022, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora
– Tanzania. Readings reproduced by FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment