"ASALI ITOKAYO
MWAMBANI”
Ijumaa, Januari 7, 2022,
1 Yoh 5:5-6, 8-13;
Zab 147: 12-15, 19-20;
Lk 5:12-16.
HAKUNA ASIYEFAA MBELE
YA YESU!
Karibuni sana wapendwa
wa Bwana kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika
somo la kwanza Mt. Yohane tunaelezwa habari kuhusu aliye na uwezo wa kuushinda
ulimwengu-ni yule aaminiye kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu. Hivyo Yesu kama mwana
wa Mungu anayo mamlaka, anao uwezo wa kutenda kadiri anavyotaka.
Yohane Uzima wote upo
katika Kristo, na hivyo tunapaswa kwenda kwa Kristo kuutafuta uzima huu.
Tukimkosa Kristo hatuwezi kusema kwamba tunao uzima. Basi tuzidi kumwamini
Kristo wetu, tusisite kumweleza shida zetu. Tatizo letu wanadamu ni kwamba
tunamrudia Kristo wakati tunapokuwa na shida tu. Hatumkumbuki mara kwa Mara.
Mara nyingi tunashindwa kuiona nguvu iliyo katika Kristo kwa sababu tunakwenda
mbele ya Kristo wakati wa ugumu tu, wakati wa raha na utulivu tunajiona
kutokumhitaji Kristo. Lakini tutambue kwamba shetani huja na kutufanyia
maangamizi wakati wa nyakati zile tunapokuwa na utulivu, au kujisikia kucheka
cheka au tukiwa na furaha. Hivi ndivyo vipindi vibaya sana kwetu kwani shetani
huja kirahisi na kutuangusha. Ndio maana baada ya raha mara nyingi hutokea
karaha kwa sababu wakati wa raha, shetani aliutumia wakati vizuri kutuangusha.
Hivyo, tuwe makini na vipindi vyetu vya anasa na furaha, ndicho kipindi
utakachoanguka na kufanya maamuzi ya ajabu. Na matendo yenye hasara kubwa sana
maishani mwako hufanyika kwa siku kama hizi.
Katika somo la injili,
Bwana Yesu anajionesha kuwa na huruma kwa kumponya aliye na ukoma. Hakika ukoma
ulimfanya mtu huyu akose raha maishani mwake na kutengwa na jamii. Kristo
anamrudishia hadhi na kumfanya akubalike ndani ya jamii zaidi. Hivyo, tusisite
kumkimbilia Yesu, kwa hakika atatuondolea ukoma wetu pia.
Ipo tabia, au kasumba
fulani ambayo inatufanya tuonekane kama ukoma kwa wenzetu. Bwana Yesu
atuondolee na kasumba za namna hiyo pia. Atusadie tuwe wanawe wapendwa, na
watumishi kwa wenzetu kwa kutuondolea tabia na udhaifu wetu unaotufanya
tuonekane kama ukoma kwa wenzetu. Pia tumwige Yesu katika tabia yake ya kusali,
wengi wetu hatuna tabia za kusali kwa wakati wote, tunasali katika matukio tu
fulani fulani, pia tunasali kwenye sherehe sherehe tu. Tumwombe Mungu tuwe na
tabia ya kusali kwa kila wakati. Tumsifu Yesu Kristo.
Copyright
©2013-20202 ©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment