“ASALI
ITOKAYO MWAMBANI”
Alahmisi,
Desemba 9, 2021,
Juma
la 2 la Majilio
Isa.
41:13-20
Mt.
11:11-15
Karibuni
sana wapendwa wa Bwana kwa tafakari ya neno la Bwana asubuhi ya leo. Bwana
Mungu wa Israeli anazidi kutoa unabii wa matumaini kwa wana wa Yuda walioko
uhamishoni Babuloni. Anawaeleza kwamba yeye ndiye Mungu, ndiye mwenye uwezo wa
kuwashika mkono, ndiye mwenye uwezo wa kuwasaidia. Hivyo wasiogope, kwani mkuu
wao ni Bwana. Anamwahidia kumfanya kama chombo kikali cha kupuria, chombo
kinachopendwa na kila mmoja kwani kinazalisha nafaka safi, Yuda atakuwa na
mamlaka tena, na sauti mbele ya watu.
Maneno
haya yanasemwa kwa Yuda wakati wakiwa utumwani, huko wapo katika shida na
wanatamani maisha ya Wababuloni, wanawaona Wababuloni kama walio barikiwa zaidi
na wenye Mungu bora. Wao wanajidharau kama waliotupwa. Nabii anawaeleza kwamba
kwa hakika wasijidharau, wao ni watu walio na thamani bora machoni pa Mungu.
Ipo siku Mungu atawakumbuka.
Ujumbe
huu utusaidie na sisi. Tuepuke kujidharau, yawezekana tukawa tunakosa fedha
mifukoni mwetu, tukakosa hata maarifa, tukawa tegemezi tu, tukakumbwa pia na
magonjwa mengi na kutudhoofisha. Lakini tutambue kwamba katika hali za namna
hiyo, bado tu wa thamani machoni pa Bwana. Hivyo tusichoke kumwamini Mungu
wetu, Mungu ni wetu pia. Mungu sio wa watu fulani fulani tu, au wenye afya,
Mungu ni baba yetu pia. Hivyo tuache kujidharau sana. Mungu sio mbaguzi kwa
watu fulani fulani tu. Mungu anazidi kuwa wetu na mwenye kutupenda hata katika
magumu yetu pia.
Katika
somo la injili, Yesu anamsifu Yohane Mbatizaji. Ni mtu ambaye maisha yake yote
aliyatolea kwa ajili ya mwingine, kumwandalia Yesu njia. Maisha yake alidiriki
hata kuishi jangwani na kula nzige na asali ya mwitu lengo likiwa ni kuwaongoza
wanadamu watubu, watazame kwamba bidhaa na biashara za jamii tunazoishi nyingi
ni haramu. Zipo zinazopatikana kwa wizi na dhuluma. Tunaposhiriki katika ulaji
wa bidhaa fulani mara nyingine tunasaidia watu waovu kuendelea kukuza biashara
zao na kupata nguvu zaidi.
Yohane
alikula chakula cha mwituni na hivyo aliweza kuepuka kuikwaza jamii kwani
hakula vitu vya dhuluma. Yohane aliishi maisha yake yote akimtengenezea Yesu
njia. Hapa alipata ukuu wake. Sisi tuwe watu wa kuwandalia njia wenzetu.
Tukiona
walio na vipaji vya mambo mbalimbali-tuwaandalie njia, tukiona wanaotaka kuishi
maisha ya utakatifu tuwaandalie njia. Kwa namna hii tutaweza kuwa wenye ukuu
katika ufalme wa Mungu kama Yohane. Pia anayewaandaa wengine wapate kumwamini
Yesu kwa mara nyingine pia hupata nafasi ya kuwa wakuu kwenye ufalme wa Mungu.
Hivyo tuwe watu wenye kukubali kuwaandalia wenzetu njia. Tumsifu Yesu Kristo.
Copyright ©2013-2020 ©FurKat,
Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment