Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA DESEMBA 9, 2021

 

 

MASOMO YA MISA DESEMBA 9, 2021

ALHAMISI, JUMA LA 2 LA MAJILIO

SOMO 1

Isa. 41:13-20

Kwa maana mimi, Bwana, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume, nikikuambia, Usiogope; mimi nitakusaidia. Usiogope, Yakobo uliye mdudu, nanyi watu wa Israeli; mimi nitakusaidia, asema Bwana, na mkombozi wako ni Mtakatifu wa Israeli. Tazama, nitakufanya kuwa chombo kikali kipya cha kupuria, chenye meno; utaifikicha milima, na kuisaga; nawe utafanya vilima kuwa kama makapi. Utawapepeta, na upepo utawapeperusha; upepo wa kisulisuli utawatawanya; nawe utamfurahia Bwana, utajitukuza katika Mtakatifu wa Israeli.

Maskini na wahitaji wanatafuta maji, wala hapana; ndimi zao zimekauka kwa kiu; mimi, Bwana, nitawasikia, mimi, Mungu wa Israeli, sitawaacha.

Nitafunua vijito vya maji juu ya vilima, na chemchemi katikati ya mabonde; nitageuza jangwa kuwa ziwa la maji, na mahali pakavu kuwa vijito vya maji.

Nitapanda katika jangwa mwerezi, mshita, mhadasi, na mbono; nitatia katika nyika mberoshi, mtidhari, na mteashuri pamoja; ili waone, na kujua wakafikiri, na kufahamu pamoja, ya kuwa mkono wa Bwana ndio uliofanya jambo hilo. Mtakatifu wa Israeli ndiye aliyeliumba.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 145:1,9-13 (K) 8

(K) Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma, Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema.

Ee Mungu wangu, Mfalme nitakutukuza,

Nitalihimidi jina lako milele na milele.

Bwana ni mwema kwa watu wote,

Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote. (K)

Ee Bwana, kazi zako zote zitakushukuru,

Na wacha Mungu wako watakuhimidi,

Wataunena utukufu wa ufalme wako,

Na kuuhadithia uweza wako. (K)

Ili kuwajulisha watu matendo yake makuu,

Na utukufu wa fahari ya ufalme wake.

Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote,

Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote. (K)

SHANGILIO

Isa. 45:8

Aleluya, aleluya,

Dondokeni, enyi mbingu toka juu, Mawingu yamwage haki; nchi na ifunuke, ili kutoa wokovu.

Aleluya.

INJILI

Mt. 11:11-15

Siku ile, Yesu aliwaambia makutano: Amin, nawaambieni, Hajaondokea mtu katika wazo wa wanawake aliye mkuu kuliko Yohane Mbatizaji; walakini aliye mdogo katika ufalme wa mbinguni ni mkuu kuliko yeye. Tangu siku za Yohane Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka. Kwa maana manabii wote na torati walitabiri mpaka wakti wa Yohane. Na ikiwa mnataka kukubali, yeye ndiye Eliya atakayekuja.

Mwenye masikio, na asikie.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristu.

 

Copyright © 2020, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment