“ASALI
ITOKAYO MWAMBANI”
Jumanne,
Desemba 7, 2021
Juma
la 2 la Majilio
Isa
40: 1-11;
Zab
95: 1-3, 10-13;
Mt
18: 12-14
MUNGU
ANATAFUTA KONDOO ALIYEPOTEA!
Karibuni
sana wapendwa wa Bwana kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la
Bwana katika somo la Injili, Bwana Yesu anatuhimiza tumkimbilie yeye, sisi sote
tunaolemewa na kusumbuliwa na mizigo na matatizo mbalimbali kwani yeye ndiye
mwenye kutupumzisha. Anatualika twende kwake, tukajivike nira yake, tukabebe
mzigo ulio wake. Wengi wetu tunabeba mizigo mizito kweli ambayo siyo mali yetu
na kwa hakika haitusaidii.
Tunajifunga
nira za ulevi, mahusiano yasiyo rafiki, tunajifunga nira na marafiki wasiokuwa
waminifu-wote hawa wametufanya tusumbuke na kulemewa na mizigo isiyo na faida.
Wengi wetu tunachoka kwa sababu ya kubeba mizigo isiyo yetu. Upo msemo wa lugha
ya kichaga usemao “Mshyahara wo isembo, ni ichoka.” Yaani, malipo ya mpumbavu
ni kuchoka bila sababu. Mpumbavu hujiingiza kwenye matukio, na visa
visivyomhusu. Hivyo mwisho wa siku hupoteza muda na rasilimali bila faida.
Yesu
ndiye mwenye kutupatia ufahamu wa kutufanya tutambue yaliyo ya muhimu na
kuyakumbatia. Tuache kukumbatia yasiyo ya muhimu. Tuondoe mizigo isiyo kuwa
yetu.
Somo
la kwanza Nabii Isaya anawaeleza wana wa Yuda walioko uhamishoni kwamba Bwana
ndiye mwenye ukuu na mwenye kuwatuliza wote na kuwapatia faraja. Hakuna
mwingine mwenye uwezo wa kufanya kama afanyavyo Bwana. Wana wa Yuda
walimfikiria mungu wa Wababuloni kama Mungu mwenye uwezo na mamlaka ya kutuliza
na kufariji kuliko Bwana Mungu wa Israeli. Lakini leo wanaelezwa kwamba hakuna
aliye kama Bwana.
Ulimwenguni
wapo wanaojidai kuwa na moyo wa kutaka kutuliza shida na matatizo yetu. Lakini
tuwe makini na hawa kwani waweza kuwa na malengo yao binafsi. Wengi
waliobembelezwa na wanadamu wameishia kutendewa unyama mkubwa. Sisi tumwamini
Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye mwenye kutubembeleza na kutufariji. Hakuna mwanadamu
au kiumbe chochote chenye uwezo wa kumzidi Bwana. Hivyo tusichanganywe au
kupoteza amani kutokana na maneno matupu ya mwanadamu mwenye kutaka
kutubembeleza. Bwana Yupo na anapaswa awe wa kwanza.
Copyright ©2013-2020 ©FurKat,
Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment