“ASALI
ITOKAYO MWAMBANI”
Jumatatu,
Desemba 20, 2021,
Juma
la 4 la Majilio
Isa
7: 10-14;
Zab
24: 1-6;
Lk
1: 26-38
MUNGU
ANAFANYA VITU VYOTE VIWEZEKANE
Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa
tafakari ya neno la Bwana asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo la kwanza
Nabii Isaya anatangaza ishara kuu, ya mtoto atakayezaliwa atakayeitwa jina la
Emmanuel, yaani Mungu pamoja nasi. Huyu ndiye atakayemsaidia mfalme Ahazi
kupambana na maadui wake, waliokuwa wakimwandama kila upande, huyu Emanuel,
Mungu pamoja nasi.
Mwenyezi Mungu anaonesha kwamba kwa hakika
pale Ahazi atakapoweza kumleta Mungu kati yao, ndipo amani
itakapopatikana kwa ufalme wake. Bwana Yesu alipozaliwa ulimwenguni,
malaika walipiga kelelele kwa furaha, wakatangaza utukufu kwa Mungu juu na
amani iwepo duniani. Yesu ndiye chanzo cha amani hii, kwani ni Mungu mwenyewe
amekuja ulimwenguni. Palipo na Mungu, palipo na Emanuel, Mungu yupo kati yao na
hakika patakuwa na amani.
Bikira Maria aliweza kupokea ujumbe wa
Malaika kwa sababu alikuwa na Mungu ndani yake. Sisi tujitahidi kuwa na Mungu
kati yetu. Hapa ndipo tutakapokuwa na amani kama mfalme Ahazi anapoelezwa leo,
kwamba ni Emanuel tu ndiye atakayeweza kumletea amani. Emanueli ni sababu ya
sisi kutulia na kuishi kwa raha na furaha zaidi. Emanueli awe sababu ya sisi
kuchanua zaidi.
Katika somo la injili, tunasikia habari za
malaika Gabrieli kutangaza juu ya kuzaliwa kwake Bwana Yesu. Gabrieli
alipokelewa na Maria kwa imani kuu kama mjumbe wa Mungu. Kwa ndio ya Maria, aliweza
kuyabariki maisha yake na maisha ya ulimwengu. Sisi tujitafakari na kutambua
kwamba mara nyingi maisha yetu tunashindwa kuyaletea baraka na pia kushindwa
kuuletea baraka ulimwengu kwa sababu ya kusema hapana kwa mapenzi ya Mungu.
Tujifunze kusema ndio kwa mapenzi ya Mungu na hapa ndipo tutakapoweza
kuyabariki maisha yetu. Mipango ya Mungu japokuwa yaweza onekana kuwa migumu
maishani mwetu kwa hakika ndiyo yatakayoleta amani na urahisi maishani mwetu.
Zaburi ya wimbo wetu wa katikati
imetuhimiza kufungua milango ili mfalme wetu, mfalme wa amani apate kuingia.
Yesu ndiye mfalme huyu. Tujifunze kusema ndio kwa mapenzi yake kama alivyofanya
Mama Maria na kwa hakika tutaweza kubarikiwa na kufurahia zaidi. Tumefunga
milango mingi kwa chuki, visasi na kutokusamehe. Tufungue ili mfalme wa amani
aingie arudishe tena amani yetu.
Copyright ©2013-2020 ©FurKat,
Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment