Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, DISEMBA 15, 2021

 

MASOMO YA MISA, DISEMBA 15, 2021

JUMATANO, JUMA LA 3 LA MAJILIO

 

SOMO 1

Isa. 45:6 – 8; 18:21 – 25

 

Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine. Mimi naiumba nuru, na kuihuluku giza; mimi nafanya suluhu, na kuhuluku ubaya; Mimi ni Bwana, niyatendaye hayo yote. Dondokeni, enyi mbingu, toka juu, mawingu na yammwage haki; nchi na ifunuke ili kutoa wokovu, nayo itoe haki ikamee pamoja; Mimi, Bwana, nimeiumba.

Maana Bwana, aliyeziumba mbingu, asema hivi; Yeye ni Mungu; ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; hakuiumba ukiwa, aliumba ili ikaliwe na watu; Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine.

Si mimi, Bwana? Wala hapana Mungu zaidi ya mimi; Mungu mwenye haki, mwokozi; hapana mwingine zaidi ya mimi. Niangalieni mimi, mkaokolewe, enyi ncha zote za dunia; maana mimi ni Mungu; hapana mwingine.

Kwa nafsi yangu nimeapa, neno hili limetoka kinywani mwangu katika haki, wala halitarudi, ya kwamba mbele zangu kila goti litapigwa, kila ulimi utaapa. Mmoja ataniambia. Kwa Bwana, peke yake iko haki na nguvu; naam, watu watamwendea yeye na wote waliomkasirikia watatahayarika. Katika Bwana wazao wote wa Israeli watapewa haki, na kutukuka.

 

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

 

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 85:8a, 9 – 13 (K) Isa. 45:8

 

(K) Dondokeni enyi mbingu, toka juu, mawingu na yamwage haki.

 

Na nisikie atakavyosema Mungu Bwana,

Maana atawaambia watu wake Amani,

Hakika wokovu wake u karibu na wamchao,

Utukufu ukae katika nchi yetu. (K)

 

Fadhili na kweli zimekutana,

Haki na Amani zimebusiana.

Kweli imechipuka katika nchi,

Haki imechungulia kutoka mbinguni. (K)

 

Naam, Bwana atatoa kilicho chema,

Na nchi yetu itatoa mazao yake.

Haki itakwenda mbele zake,

Nayo itazifanya hatua zake kuwa njia. (K)

 

SHANGILIO

Isa. 40:9 – 10

 

Aleluya, aleluya,

Paza sauti kwa nguvu, Wewe uhubiriye habari njema; Tazameni, Bwana Mungu atakuja kama shujaa.

Aleluya.

 

INJILI

Lk. 7:19 – 23

 

Siku ile, Yohane aliwaita wawili katika wanafunzi wake, akawatuma kwa Yesu, akiuliza, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine? Nao walipofika kwake, walisema, Yohane Mbatizaji ametutuma kwako, akisema, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine?

Na saa ile ile aliwaponya wengi magonjwa yao, na misiba, na pepo wabaya; na vipofu wengi aliwakirimia kuona. Ndipo alipojibu, akawaambia, kuyasikia; vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakasika, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, maskini wanahubiriwa habari njema. Naye heri mtu yeyote asiyechukizwa nami.

 

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

                                    

 

Copyright © 2020, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment