MASOMO YA MISA DESEMBA 31, 2021
IJUMAA, OKTAVA YA NOELI
SOMO 1
1Yoh. 2:18-21
Watoto, ni wakati wa mwisho; na
kama vile mlivyosikia kwamba mpinga Kristo yuaja, hata sasa wapinga Kristo
wengi wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho.
Walitoka kwetu, lakini hawakuwa wa kwetu. Maana kama wangalikuwa wa kwetu, wangalikaa
pamoja nasi. Lakini walitoka ili wafunuliwe kwamba si wote wa kwetu. Nanyi
mmepakwa mafuta na Yeye aliye Mtakatifu nanyi mnajua nyote. Sikuwaandikia ninyi
kwa sababu hamwijui iliyo kweli, bali kwa sababu mwaijua, tena kwamba hapana
uongo wowote utokao katika hiyo kweli.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 96:1-2, 11-13 (K) 11a
(K) Mbingu na zifurahi, nchi na
ishangilie.
Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Mwimbieni Bwana, nchi yote.
Mwimbieni Bwana, libarikini jina
lake,
Tangazeni wokovu wake siku kwa
siku. (K)
Mbingu na zifurahi, nchi na
ishangilie,
Bahari na ivume na vyote
viijazavyo,
Mashamba na yashangilie, na vyote
vilivyomo,
Ndipo miti yote ya mwituni iimbe
kwa furaha;
Mbele za Bwana, kwa maana anakuja,
Kwa maana anakuja aihukumu nchi.
(K)
Atauhukumu ulimwengu kwa haki,
Na mataifa kwa uaminifu wake. (K)
SHANGILIO
Ebr. 1:1-2
Aleluya, aleluya!
Baada ya Mungu kusema zamani mara
nyingi na kwa namna ningi na baba zetu kwa kinywa cha manabii, siku hizi zilizo
za mwisho amesema nasi kwa kinywa cha Mwana.
Aleluya.
INJILI
Yn. 1:1-18
Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye
Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa
Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika chochote
kilichofanyika. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya
watu. Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza.
Palitokea mtu, ametumwa kutoka kwa
Mungu, jina lake Yohana. Huyo alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru,
wote wapate kuamini kwa yeye. Huyo hakuwa ile nuru, bali alikuja ili aishuhudie
ile nuru.
Kulikuwako Nuru halisi, amtiaye
nuru kila mtu, akija katika ulimwengu. Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye
ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua. Alikuja kwake, wala
walio wake hawakumpokea. Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika
watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala
si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu. Naye Neno
alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa
mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.
Yohana alimshuhudia, akapaza sauti
yake akasema, Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Ajaye nyuma yangu
amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu.
Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi
sote tulipokea, na neema juu ya neema. Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa
Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo. Hakuna mtu aliyemwona
Mungu wakati wowote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye
aliyemfunua.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee
Kristu.
Copyright © 2020, "MASOMO YA
MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings
reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment