MASOMO YA MISA DESEMBA 30, 2021
SIKU YA SITA YA OCTAVA YA KUZALIWA
BWANA
SOMO 1
1Yoh. 2:12-17
Nawaandikia ninyi, watoto wadogo,
kwa sababu mmesamehewa dhambi zenu, kwa ajili ya jina lake. Nawaandikia ninyi,
akina baba, kwa sababu mmemjua yeye aliye tangu mwanzo. Nawaandikia ninyi,
vijana, kwa sababu mmemshinda yule mwovu. Nimewaandikia ninyi, watoto, kwa
sababu mmemjua Baba. Nimewaandikia ninyi, akina baba, kwa sababu mmemjua yeye
aliye tangu mwanzo. Nimewaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mna nguvu, na neno
la Mungu linakaa ndani yenu, nanyi mmeshinda yule mwovu.
Msiipende dunia, wala mambo
yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake.
Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na
kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita,
pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 96:7-10 (K) 11a
(K) Mbingu na zifurahi, nchi na
ishangilie
Mpeni Bwana, enyi jamaa za watu,
Mpeni Bwana utukufu na nguvu,
Mpeni Bwana utukufu wa jina lake.
(K)
Leteni sadaka mkaziingie nyua zake,
Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa
utakatifu,
Tetemekeni mbele zake, nchi yote.
(K)
Semeni katika mataifa, Bwana
ametamalaki;
Naam, ulimwengu umethibitika
usitikisike,
Atawahukumu watu kwa adili. (K)
SHANGILIO
Aleluya, aleluya
Siku takatifu imetung’aria: Enyi
mataifa njoni mkamwabudu Bwana: Kwa sababu mwanga mkubwa umeshuka duniani.
Aleluya.
INJILI
Lk. 2:36-40
Siku ile palikuwa na nabii mke,
jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka
mingi alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake. Naye ni mjane
wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na
mchana kwa kufunga na kuomba. Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na
wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake.
Basi, walipokwisha kuyatimiza yote
kama yaliyoagizwa katika sheria ya Bwana, walirejea Galilaya, mpaka mjini kwao,
Nazareti. Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya
Mungu ilikuwa juu yake.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee
Kristu.
Copyright © 2020, "MASOMO YA
MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings
reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment