MASOMO YA MISA, DESEMBA 12, 2021
DOMINIKA YA 3 YA MAJILIO MWAKA C WA KANISA
MWANZO:
Flp. 4:4,5
Furahini katika Bwana siku zote; tena nasema furahini. Bwana yu karibu.
SOMO 1
Sef. 3:14-18
Imba, Ee binti Sayuni; piga kelele, Ee Israeli; Furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, Ee binti Yerusalemu. Bwana ameziondoa hukumu zako, amemtupa nje adui yako; Mfalme wa Israeli, naam, yeye Bwana, yu katikati yako; hutaogopa uovu tena. Katika siku ile Yerusalemu utaambiwa, Usiogope, Ee Sayuni; mikono yako isilegee. Bwana, Mungu wako, yu katikati yako, shujaa awezaye kuokoa; Atakushangilia kwa furaha kuu, atatulia katika upendo wake. Atakufurahia kwa kuimba. Nitawakusanya wanaousikitikia mkutano wa ibada, hao waliokuwa wa kwako.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Isa. 12:2-6 (K) 6
(K) Paza sauti, piga kelele maana mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako.
Tazama, Mungu ndiye wokovu wangu;
Nitatumaini wala sitaogopa;
Maana Bwana ni nguvu zangu na wimbo wangu.
Naye amekuwa wokovu wangu.
Basi, kwa furaha mtateka maji
Katika visima vya wokovu. (K)
Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake;
Yatangazeni matendo yake kati ya mataifa
Litajeni jina lake kuwa limetukuka. (K)
Mwimbieni Bwana, kwa kuwa ametenda makuu;
Na yajulikane haya katika dunia yote.
Paza sauti, piga kelele, mwenyeji wa Sayuni;
Maana Mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako. (K)
SOMO 2
Flp. 4:4-7
Ndugu zangu: Furahini katika Bwana siku zote; tena nasema, Furahini. Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu. Msijisumbue kwa neno lolote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
SHANGILIO
Lk. 4:18
Aleluya, aleluya,
Roho wa Bwana yu juu yangu, amenituma kuwahubiri maskini habari njema.
Aleluya.
INJILI
Lk. 3:10-18
Siku ile: Makutano wakamwuliza Yohane Mbatizaji, Tufanye nini basi? Akawajibu akawaambia, Mwenye kanzu mbili na ampe asiye na kanzu; na mwenye vyakula na afanye vivyo hivyo. Watoza ushuru nao wakaja kubatizwa, wakamwuliza, Mwalimu, tufanye nini sisi? Akawaambia, Msitoze kitu zaidi kuliko mlivyoamriwa. Askari nao wakamwuliza, wakisema, Sisi nasi tufanye nini: akawaambia, Msidhulumu mtu, wala msishitaki kwa uongo; tena mtoshewe na mshahara wenu.
Basi, watu walipokuwa wakingoja yatakayotokea, wote wakiwaza-waza mioyoni mwao habari za Yohana, kama labda yeye ndiye Kristo, Yohane alijibu akawaambia wote, Kweli mimi nawabatiza kwa maji; lakini anakuja mtu mwenye nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuulegeza ukanda wa viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto; ambaye pepeo lake li mkononi mwake, naye atausafisha sana uwanda wake, na kuikusanya ngano ghalani mwake, bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika. Basi, kwa maonyo mengine mengi aliwahubiri watu.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
No comments:
Post a Comment