Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

KUISIKILIZA SAUTI YA MUNGU!

 

“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”

Jumamosi, Desemba 4, 2021,

Juma la 1 la Majilio

 

 

Isa 30: 19-21, 23-26;

Zab 147: 1-6;

Mt 9:35 - 10: 1, 6-8

 

 

KUISIKILIZA SAUTI YA MUNGU!

Ndugu zangu karibuni katika adhimisho la Misa Takatifu. Nabii Isaya katika somo la kwanza anatabiri ujio wa ukombozi kwa taifa la Yuda liloloko utumwani Babiloni. Nabii anatangaza kwamba uovu wake umeachiliwa. Hapa nabii anaonesha kwamba lengo la uhamisho lilikuwa ni kulisafisha na kulitakasa taifa la Yuda na si kuliangamiza.

Katika injili ya leo, Yesu anaendeleza ujumbe huu kwa mapana zaidi anapopita katika miji na vijiji kuwaongoa na kuwaponya wale waliokuwa katika utumwa wa magonjwa. Kuwatoa katika Babiloni ya dhambi, magonjwa, kufungwa na pepo na kuwaleta katika Yerusalemu ya afya njema na furaha.

Yesu anawapa pia mitume wake kazi hiyo hiyo kwa kuwatuma wakafanye kama yeye alivyofanya, lakini anawaambia “wamwombe Bwana wa mavuno”, kwa njia nyingine Yesu anawaambia wasali kwa Baba, wawe na Imani ili kazi yao ibarikiwe na wafanikiwe na Mungu aongeze watenda kazi.

Hivi ndivyo mawazo ya Yesu kwa mwanadamu yalivyo mapana. Lengo lake ni kutuokoa na pale anapotuadhibu anataka tutakasike. Hivyo, hali tukisubiri siku yetu ya mwisho na ujio wa Yesu kwa mara ya pili, tuige mfano wa Yesu. Tuwe na malengo mapana. Tuwaongoe watu katika dhambi na kuwaleta kwa Mungu. Tusivumilie kukaa na wazinzi, waregevu, walevi na walafi bila kuwaongoa. Na tutaweza kufanya hivi kama tutakuwa na Imani na kusali kwa Bwana wa mavuvo, Baba.

Tusali kwa Yesu tukimwambia, Ee Yesu nisamehe kwa pale nilipowakwaza wenzangu na kushindwa kuwaongoza kwako, kwasababu ya kukosa Imani Amina!

 

Copyright ©2013-2020 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment