“ASALI
ITOKAYO MWAMBANI”
Jumanne,
Desemba 14, 2021,
Juma
la 3 la Majilio
Sef
3: 1-2, 9-13;
Zab
34: 2-3, 6-7, 17-19, 23;
Mt
21: 28-32
JE,
WEWE NI MDHAMBI?
Somo
la leo kutoka katika kitabu cha nabii Sefania, linatoa onyo na ole kwa wale
wanaokataa kusahihishwa, wanaokataa kusikia, na kuitika wito wa kumwamini
Mungu. Katika somo la Injili, Yesu anasema kwamba ‘Watoza ushuru na wenye
dhambi wataingia katika Ufalme wa Mungu kabla ya viongozi wa dini’. Je, ni
kweli kwamba watoza ushuru na wenye dhambi waliingia katika Ufalme wa Mungu
kabla ya viongozi wa dini ya Wayahudi? Je, Yesu alikuwa anasema kweli kwamba
utakatifu wa watoza ushuru na makahaba ulizidi ule wa viongozi wa dini? Ndio,
ilikuwa hivyo kwasababu majivuno yaliwafanya viongozi wa dini kuwa na moyo
mgumu wa kupokea ujumbe wa Ufalme wa Mungu alioleta Yesu mwenyewe kwa maneno
yake. Walifikiri juu ya ukubwa wao sana na walipenda wengine wawaze juu ya
ukubwa wao. Walikuwa wamejiridhisha wenyewe kwa utakatifu wao wenyewe,
nakujiona wema kabisa, jambo ambalo ni mbaya kweli. Lakini Yesu anayaona yote
hayo, na anawanyanyua watoza ushuru na wenye dhambi kwa utayari wao wakutubu na
kumpokea, Yesu anawapandisha kwenye thawabu ya Ufalme wa Mungu.
Tujitafakari
sisi wenyewe kama tunamfanano na tabia ya viongozi wa dini wa Wayahudi wa
kipindi hicho au tuna tabia ya hawa watoza ushuru na wenye dhambi waliokubali
kupokea maneno ya Yesu. Pengine, ni vigumu kukubali. Pengine tumejitengenezea
tabia ya kujitambulisha sisi wenyewe kama watu wazuri na wasio na kosa na wenye
haki. Yesu anataka tujione wenyewe katika kundi hili la watoza ushuru na wenye
dhambi. Hii ni kwasababu sisi wote ni wadhambi. Tunaweza tusiwe katika hali ya
kuumia moyoni kama wao walivyoumia, lakini ukweli ni kwamba tunaumia kwasababu
ya dhambi zetu, tunapaswa kukiri hili. Na kwakweli, kama tunashindwa kukubali
dhambi zetu na madhaifu yetu, hatuna tofauti na viongozi hawa wa dini ya
Kiyahudi. Tutakuwa tumebaki katika majivuno yetu na kujihesabia haki wenyewe.
Sala:
Bwana, jaza moyo wangu kwa unyenyekevu. Na kwa unyenyekevu, naomba unisaidie
niweze kujiona mwenyewe kama nilivyo. Nisaidie niweze kuona dhambi yangu lakini
pia unisaidie kuona juhudi zangu za kukutafuta. Nisaidie niweze kuacha dhambi
zangu nikurudie ili niweze kufurahia furaha na uhuru wa kuingia katika Ufalme
wako. Yesu, nakuamini wewe. Amina.
Copyright ©2013-2020 ©FurKat,
Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment