ASALI
ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari
ya kila siku
Jumatatu,
Novemba 22, 2021,
Juma
la 34 la Mwaka wa Kanisa
Dan
1:1—6,8-20;
Lk
21: 1-4.
Karibuni
ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana
tunalokutana nalo katika asubuhi ya leo ni la matumani na linatuambia kwamba
Bwana huhukumu kwa kufuata moyo na hili analionyesha anavyoisifia ile sadaka
kidogo inayotolewa na huyu Mama mjane leo. Mama huyu alitoa ile senti ya mwisho
iliyokuwa inalinda nyumba yake, yaani hakubakiwa na kitu, yaani aliutoa moyo
wake wote kwa Bwana na hili ndilo Bwana analotaka; yaani imani yako uweke na
matumaini yako kwake. Yeye anajua kwamba kuna wengine waliokuwa wanatoaga
mamilioni lakini imani yao kwake ilikuwa mbali kabisa. Fundisho lake hapa ni
kwamba unapotoa sadaka yoyote, hakikisha moyo wako upo katika ile sadaka, yaani
umejichunguza tayari, umeshajizatiti natoa hiki na hiki kwa ajili ya nini, na
unakuja kanisani ukijua kwamba nampa Bwana hiki kitu kwa sababu gani-yaani moyo
wako uwe pale.
Kosa
la wale matajiri ni kwamba walipokuwa wanatoa, moyo wao haukuwa kwenye ile
sadaka, yaani hawakutoa mioyo yao bali walienda tu kama sehemu tu ya
kujionyesha onyesha-mioyo yao haipo kwenye sadaka yao kabisa. Hawajiuliza hata
juu ya sababu za wao kutoa sadaka-ni sehemu ya kujionyesha au kufanyia matanuzi
yao na hiki ndicho anachokiona Yesu.
Hapa
anatufundisha kwamba katika yote mtakayofanya kwa ajili ya Bwana, usiamke tu na
kuja na kuwaona wenzako wanaamka na kutoa au kuja kanisani na wewe unakimbilia
na kuunga tela na kumbe hata moyo wako haupo. Wewe jichunguze kwanza na
hakikisha hata kama ni sadaka yako ya kanisani, moyo wako uwe kwenye hiyo
sadaka-jiulize kwa nini unatoa na sababu za kutoa na muombe Mungu akutimizie
Baraka zake.
Na
katika somo la kwanza tunakutana na mfano wa kijana Daniel na wenzake ambaye
moyo wake wote ulibakia bado kwa Bwana, licha ya yeye kuwa katika nchi ya
kigeni, akili yake yote bado ilibakia Yerusalem, katika dini yake aliyoiacha.
Na leo anakataa kula chakula cha mfalme kwa sababu tu ya kukumbuka dini na
tamaduni zake kule nyumbani, hataki kujinajisi kabisa-ikitegemea kwamba baadhi
ya vyakula vya wapagani havikupokelewa na tamaduni za Kiisraeli. Kila
akikumbuka dini yake moyo wake uliwaka.
Hapa
ndugu zangu tunafundishwa kwamba mioyo yetu iwe juu ya vile tulivyovichagua.
Hata unapotoa kitu kwa ajili ya Bwana-moyo wako uwe pale. Usiingie tu na
kuokota mia mbili iliyoanguka uvunguni na kuitoa tu. je, jiulize moyo wangu uko
kwenye hii mia mbili na ninapoitoa hii mia mbili-moyo wangu umeambatana nayo?
Na
hata unapokuja kanisani, jiulize moyo wangu umeambatana na hapa kanisani au la?
Na hata kama upo katika ndoa au utawa-jiulize moyo wangu umeambatana na huu
utawa? Hivyo, mioyo yetu iambatane na makusudio yetu.
Copyright ©2013-2020 ©FurKat,
Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment