Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

UPO TAYARI KUMSHANGAZA YESU?

 

“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”

Jumatatu, Novemba 29, 2021

Juma la 1 la Majilio

 

Isa 2:1-5;

Zab 122:1-9;

Mt 8: 5-11.

 

 

UPO TAYARI KUMSHANGAZA YESU?

 

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo ambapo tupo katika kipindi cha majilio. Neno la Bwana linaanza kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo tunamkuta nabii Isaya anatabiri juu ya ujio wa nyakati za neema kwa mji wa Yerusalem ambapo falme zote za mataifa zingeuendea ili zipate neema, ili zimtambue Mungu wa kweli na kubarikiwa. Anasema kwamba vitu kama vita havitasikika tena ndani ya mji huo na watu hawatajiandaa tena kwa ajili ya mapigano. Ndugu zangu, wakati nabii huyu anatoa unabii huu, taifa hili lilikuwa linajiandaa kwa ajili ya mapigano kati yake na taifa la Waasiria na baadhi ya Wayahudi waliogopa wakifikiri kwamba hawa jamaa wangewamaliza. Lakini nabii anawapa moyo. Anasema kwamba wasistushwe na hivi vita. Wakati utafika ambapo hawa wanaotafuta kupigana nao watajikuta wakija Yerusalem na kuja kutafuta huko Mungu wa kweli na watu hawatajiandaa tena na vita.

Ndugu zangu, tukiiangalia injili ya leo, tunagundua kwamba nyakati hizi zilitokea. Hii ni kwa sababu kwa ujio wa Yesu, watu wa mataifa mengine, kama huyu Akida wa Kirumi tunayemsikia leo anadiriki kuja Yerusalemu, anakwenda kwa Yesu akijua kwamba wokovu unapatikana huko na huko anapata nafasi ya mtumwa wake kuponywa ugonjwa wake. Ama kweli, watu kutoka katika kabila zote na mataifa yote walikuja Yerusalemu kwa Yesu kutafuta wokovu.

Yeye aliyefanya haya yote kwa ujio wake wa kwanza, atakapokuja mara ya pili atatukaribisha katika Yerusalemu mpya, yaani mbinguni kwenye mlima mtakatifu. Na huko atatuonyesha Mungu wa kweli na huko tutakaa tukimtumikia Mungu milele.

Basi katika kipindi hiki tujiandae vyema kwa ujio Mwokozi wetu. Tujiandae tena kwa ujio wake wa pili. Sakramenti ya kitubio ndio sakramenti pekee ambayo kwayo sisi twaweza kujiandaa vyema na kustahili kusimama mbele ya Mungu siku ya ujio wake wa pili. Dhambi zetu zitatuzuia kusimama mbele ya Mungu.

Kuwakumbuka wenye shida katika kipindi hiki ni namna nzuri pia ya kujiandaa katika kipindi hiki. Tumsifu Yesu Kristo.

Copyright ©2013-2020 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

 

No comments:

Post a Comment