Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

UPENDO WA KWELI UNASHINDA HOFU

 

“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”

Tafakari ya kila siku

Ijumaa, Novemba 26, 2021,

Juma la 34 la Mwaka

 

Dan 7: 2-14;

Dan 3: 75-81 (K) 59;

Lk 21: 34-36.

 

 

UPENDO WA KWELI UNASHINDA HOFU

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika asubuhi ya leo linatupeleka kutafakari juu ya ujio wa nyakati za mwisho na lugha inayotumika katika masomo yote mawili ni lugha ya kiufunuo. Somo la kwanza, Danieli anaelezea (kwa mfano wa wanyama wanne, wanyama kutoka kuzimu) uwepo wa tawala nne zilizojivuna sana, zilizoua watu wa Mungu, zilizowatesa Wayahudi. Danieli anaelezea kwamba hawa wote watakwisha na mamlaka yatakabidhiwa kwa yule aliye mfano wa Mwanadamu. Anaonyesha mamlaka yote yako chini ya Mungu na yeye anamiliki kila kitu. Hukuna mamlaka iliyo juu yake. Hapa, Danieli anawaonya Wayahudi kwamba wasije wakajipendekeza kwa watawala Fulani Fulani na wanasiasa dunia na kuwashabikia kama miungu na kuona kwamba ati hawashindwi. Siku za mamlaka yao zinahesabika tu. Aliye na mamlaka ni Mungu.

 

Injili ya leo inaendeleza ujumbe huu kwa kusisitiza kwamba maisha ya mkristo ni mkesha akipambana kujiweka mikononi mwa Mungu. Na katika mkesha huu, anahitaji hekima kubwa. Hekima ya kuweza kusoma alama za nyakati. Hekima itakayomwezesha kuyatazama yote yanayotendeka ulimwenguni kwa macho ya kimungu na hivyo kupambanua wakati na tendo la kufaa kwa wakati. Mwenye macho ya kimungu atamuona omba omba kama Yesu anayeomba mahitaji, au vitu kama matetemeko ya ardhi kama sehemu ya Yesu akiwaalika watu watubu. Asiye na macho ya kimungu atamuona ombaomba kama msumbufu au mvivu. Anayejikabidhi mikononi mwa Mungu kwa njia ya sala ndiye mwenye kuipokea hekima hii kwani anayetenda si yeye bali ni roho ya Bwana aliyeko ndani yake na husafiri naye kumwonyesha kumfanya asiaibike kamwe.

 

Ndugu zangu, nyakati zetu hizi tunahitaji sana macho ya kimungu. Tunahitaji kusafiri na Bwana Zaidi na Zaidi na kujifunza toka kwake. Tunahitaji Bwana atende ndani yetu, aziongoze familia zetu, kazi zetu, na matamanio yetu. Atufundishe kuachana na tamaa mbalimbali.

 

Atukumbushe tena kwamba Kristo anapatikana katika wadogo-hili ni la muhimu sana. Atukumbushe kwamba Kristo anapatikana ndani ya wale ambao tunawadharau, wale ambao inakuwa vigumu kusikiliza chochote toka kwao. Sasa tunamhitaji Kristo atufundishe thamani ya watu hawa kwani sisi tunakuwa vigumu kuwapokea na kuona Kristo ndani yao.

 

 

 

Copyright ©2013-2020 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment