Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

SUBIRA, UVUMILIVU UTAKUSHINDIA MAISHA!

 

“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”

Tafakari ya kila siku

Jumatano, Novemba 24, 2021.

Juma la 34 la Mwaka

 

Dan 5: 1-6, 13-14, 16-17, 23-28;

Dan 3: 62-67 (K) 59;

Lk 21: 12-19.

 

 

SUBIRA, UVUMILIVU UTAKUSHINDIA MAISHA!

 

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana katika asubuhi ya leo linatukumbushia juu ya ujio wa nyakati za mwisho ambazo zitajawa na vishawishi vingi na vitu vya kuchanganyachanganya na hivyo itawahitaji sisi kama Wakristo kuwa makini Zaidi.

 

Katika somo la kwanza, tunakutana na mfalme Belshazzar akipewa adhabu kali kabisa. Anauawa na ufalme wake unapotea kabisa na ilitokana na yeye kumkosea Bwana Mungu wa Israeli heshima. Yeye alitumia vyombo vya hekalu vilivyoletwa na baba yake kule hekaluni Yerusalem na kuvitumia na kuvinajisi;hakumpatia Bwana Mungu wa Israeli utukufu na yalimpata haya yote, anaona maajabu makubwa na mkono wa Mungu unakuja na kumwandikia adhabu yake na kwa sababu alikuwa hajajiandaa na alitawaliwa na majivuno, alikufa mwishowe-hakutumia maisha yake kumpatia Bwana Mungu utukufu na heshima bali alitaka aupate yeye.

 

Yesu katika injili anawaonya wanafunzi wake juu ya ujio wa nyakati ngumu za maisha magumu hasa kwa wale watu wa Imani. Jana tulisikia juu ya matetemeko na njaa, na vita, vyote hivi vitatokea. Na leo wanaambiwa tena kwamba watakamatwa na kuteswa na kupelekwa mbele ya masunagogi. Anawaambia kikitokea kipindi kama hiki, kinatakiwa kiwe kipindi cha wao kuonyesha Imani yao zaidi na zaidi na sio kipindi cha kupoteza Imani. Wakionyesha Imani watapewa hekima ambayo hata watesi wao hawataweza kuipata. Hivyo, nyakati kama hizi ni nyakati za kumtumainia Mungu zaidi na zaidi.

 

Katika masomo yetu, haya tunaambiwa kwamba kumtumikia Mungu ni kila wakati. Hakuna wakati wa kusema ati mimi napumzika, au wakati huu hauruhusu kwa sababu hatari ni kubwa na hivyo unaaamua kujiunga na malimwengu na dhambi kwani wakati huu ni wakati wa kujiunga na dhambi. Hapa ndugu yangu sio hivyo, maisha ya ushuhuda ni kila siku.

 

Na kabla Yesu hajaja ile siku yake ya mwisho, inatakiwa tukute tumeshaishi ushuhuda vya kutosha, tumeshamtangaza kwa kila mtu, ili hata Mungu akitaka kumlaumu mtu ukute kwamba lawama yake ni ya haki na si kumlaumu mtu ambaye hata injili haikuwahi kumfikia kwa sababu nyie mliopewa jukumu la kuihubiri injili hamkufanya sehemu yenu.

 

Hivyo sifa ni mali ya Mungu na hivyo tumwachieni Mungu hizo sifa jamani. Hicho ndicho kilicho cha muhimu. Sifa ni za Mungu, zimpatie Mungu hizo sifa, hakikisha ukiwa hapa duniani Mungu anapata sifa kupitia kwako, usikubali mwingine akwazike kwa namna yoyote ile. Tuwafundishe wote mwenendo mwema.

 

Na wale ambao kati yetu tunaheshimiwaga sana na kutukuzwa kama miungu lazima kuwa makini kidogo. Nakwambia lazima tufahamu kwamba sifa nyingine tunapata kwa ajiili ya Yesu na hivyo wewe ukizipewa mfanye Yesu azipate katika hali ya ukuu Zaidi jamani. Hili ni la muhimu sana. Usijidai kuzichukua kama Belshazar na kuzifungia wewe ukijidai ati ni zako; utaangamia vibaya. Lakini hata hivyo ni bora kujiuliza, hizi sifa napewa kwa ajili ya Yesu! na je? Nipo na Yesu? Au Yesu yupo Kilometa 200?

 

Tujifunze pia vitu vitajatifu sio vya kuchezea, lazima viwe na sehemu yake ya heshima, Biblia, rosary nk, viheshimiwe na vitengewe sehemu yake maalumu ya kuviweka sio kuvitupatupa. Ingefaa katika nyumba yako tenga mahali pakuhifadhi vitakatifu au visakramenti. Vitu vya Mungu viheshimiwe

 

Copyright ©2013-2020 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

 

No comments:

Post a Comment