Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

Sisi tuige mfano wa mzee Eleazari

 

Tafakari ya kila siku

Jumanne, Novemba 16, 2021.

Juma la 33 la Mwaka wa Kanisa

 

2 Mak 6: 18-31;

Lk 19: 1-10

 

Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo la kwanza Bwana anatupatia habari za kifo dini cha Mzee Eleazari. Huyu alikuwa mzee maarufu, mwenye heshima zake kwa Uyahudi wote.

Lakini kwa siku ya leo Mfalme Antiokus anaamua kumwaibisha hadharani, anamweleza aende kinyume na desturi zake takatifu, afanye kitu kilicho kinyume na desturi za dini yake. Naye anakataa kwani anajua kwamba haishi ili awe kibaraka wa wafalme wa dunia bali yeye maisha yake yanapaswa yamtumikie Bwana. Hivyo anakataa kuwa kibaraka wa Mfalme, kwa kukataa kuvunja desturi za dini yake.

Kishawishi kinachompata Eleazari kinafanana na kishawishi alichokipewa Yesu na shetani kwamba amsujudie na hapo atamkabidhi yote. Yesu alikishinda kishawishi hiki kwa kuonesha kwamba hapaswi kuwa kibaraka wa shetani au wa falme za kidunia. Eleazari alitambua kwamba ikiwa atakuwa kibaraka wa mfalme wa kipagani, hakika ataacha mfano mbaya kwa kizazi kijacho. Hakuna atakayeheshimu dini ya Kiyahudi na pia vijana wengi wangeiga mfano wake mbaya na kuangusha tamaduni za Kiyahudi na hakika kwa kosa lake, angeiachia dunia mfano mbaya. Aliamua kuvumilia mateso na mateso yale yaliiokoa maisha yake na kuisaidia dini ya Kiyahudi iendelee kustahimili vyema mapigo toka kwa watesi wao.

Sisi tuige mfano wa mzee Eleazari. Tujue kwamba maisha yetu yanapaswa kuwa mfano. Tusisite kuwa shahidi kwa ajili ya Kristo. Tendo moja la kisadaka lenye kuitetea imani yetu litaikuza imani yetu kwa kiasi kikubwa sana. Maadili ya dini yetu yanapuuzwa sehemu nyingi kwa sababu sisi wenyewe hatujali na hatupo tayari kujitolea sadaka kwa ajili ya Kristo.

 

Pia baadhi yetu ni watu wa njaa, tunathamini fedha kuliko maadili ya dini yetu. Rushwa yaweza ikaonekana kwamba inanifaidisha mimi lakini kwa kiasi kikubwa inaimomonyoa jamii ya kesho na kuifanya ipotee zaidi.

Kwenye somo la injili, Zakeyo anakuwa tayari kupanda juu ya mti ili apate kumwona Yesu. Na alipopanda juu ya mti, Yesu aliweza kumwona na kumtambua mara moja na huu ukawa mwanzo wake wa kubadilika.

Tujichunguze na sisi pia. Labda tupo kama Zakayo. Kazi tunazofanya na mazingira tunayokaa yanatuzuia kukutana na Yesu. Lazima tufanye kama Zakayo, tupande juu na hapo tutaweza kuonana na Yesu vyema. Hivyo tuchunguze mazingira yetu, wakati mwingine ndiyo kikwazo kinachotuzuia tushindwe kuonana na Yesu.

Pia maneno yetu, ndiyo kikwazo kinachotuzuia tushindwe kuonana na Yesu. Pia baadhi ya marafiki-yaweza wakawa ndio kikwazo kinachonifanya nishindwe kukutana na Yesu. Panda juu ya mti kama Zakeyo na hivyo uonane na Yesu. Waache kukuzuia.

Copyright ©2013-2020 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment