“ASALI
ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari
ya kila siku
Jumamosi,
Novemba 20, 2021.
Juma
la 33 la Mwaka
Jumamosi,
kumbukumbu ya Bikira Maria.
1Mak
6: 1-3;
Zab
9: 1-3, 5, 15, 18 (K) 15;
Lk
20: 27-40.
MUNGU
WA WALIO HAI
Karibuni
ndugu zangu kwa adhimisho la Misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana
linaanza kwa kuliangalia somo la kwanza kutoka katika kitabu cha Wamakabayo.
Sasa tunakutana na habari za mfalme Antiokus Epiphanes na leo anajuta kwa
sababu mambo yamekuwa magumu. Huyu mfalme hakuwa Myahudi bali alitoka taifa la
Wagiriki na hivyo aliwatesa sana Wayahudi. Alitaka kuangamiza dini yao kabisa
na kuwafanya waabudu miungu na tamaduni za Kigiriki na alipitisha amri kusema
kwamba Myahudi yeyote atakayekutwa akifuata tamaduni za Kiyahudi auawe. Hivyo,
aliwauwa sana Wayahudi wote waliokataa kukubaliana naye. Alidiriki hata
kuingiza sanamu za miungu ya taifa la wagiriki ndani ya hekalu la Wayahudi huko
Yerusalem ili waisraeli waache kumwabudu Mungu wao na kuabudu hayo masanamu.
Uovu wa huyu Antiokus ulikuwa mkubwa sana kiasi kwamba nabii Danieli katika
kitabu chake alimwelezea kama limnyama lililotumwa na shetani ili
liwangatengate watu wa Mungu.
Baadhi
ya Wayahudi waliogopeshwa na nguvu zake na ushujaa wa huyu kiongozi na hivyo
walikubali kuitumikia hii miungu ya Kigiriki. Lakini baadhi walikimbilia
mlimani-msituni na kuanza kupambana naye. Hawakuchoka bali walipambana naye kwa
miaka arobaini na kila siku huyu mfalme nguvu zake na ukatili wake ulikuwa
unaongezeka. Lakini chaajabu ni kwamba, leo katika somo la kwanza, huyu mfalme
baada ya miaka yote ya ubabe anashindwa. Nguvu zake kwisha kazi. Wale Wayahudi
waliokimbilia msituni na kuanza kupambana na huyu mfalme wa Kigiriki
wanashinda, wanauteka mji wao wa Yerusalem, wanaingia na kuvunjavunja lile
lisanamu la miungu ya Kigiriki lililowekwa ndani ya hekalu na kulitakasa tena
hekalu. Yule mfalme anabakia akijutia kama tulivyosikia katika somo la kwanza
akisema angalau nisingewafanyia Wayahudi hivyo na huu unakuwa mwisho wake na
watu wa Bwana wanashinda na miungu ya Kigiriki inavunjwa vunjwa kabisa.
Hapa
tuna cha kujifunza ndugu zangu; Unapotumia uovu wako kuwadhulumu watu, jua
kwamba midomo ya unaowadhulumu nayo inasali kumlilia Mungu na nakwambia muda
utafika ambapo mambo yatakugeukia. Somo hili tena ni onyo kwetu kwamba tuache
kasumba ya kufikiri kwamba usalama unapatikana kwa pale ninapokuwa na mkubwa
Fulani akinikingia kifua, akinipigania. Anayeweza kukukingia kifua ni Yesu
mwenyewe kwani hawa binadamu wengine wanafaulu kidogo tu lakini mwisho wa siku
nao wanateketea kama akina Antiokus.
Katika
somo la injili tumesikia habari juu ya Wasadukayo ambao hawakuamini juu ya
ufufuko. Hawa walitumia muda wao wote ili kukusanya mali za kutosha na kuishi
kwa raha wakifikiri kwamba maisha huishia hapahapa na leo wanampatia Yesu hili
swali ili kumtega ili kumwonyesha jinsi suala la ufufuko lisivyowezekana na
hata kama yatakuwako basi yatakuwa ni maisha ya vita tu kwani maadui wako wote
nao utawakuta huko mbinguni na huko mtaanza kupigana tena. Yesu anakataa na
kusema maisha ya baadaye ni tofauti na hapa duniani kwani kule kuna kuishi
kitakatifu. Na maisha yote ya duniani, yawe ya ndoa, utawa lengo lake ni
kukufanya umfikie Mungu na si kutimizia tamaa za kimwili. Mke au baba unayeishi
naye lengo la kwanza ni ili akusaidie ufike kwa Mungu. Hivyo, unapokuwa katika
ndoa, lazima ujiulize kwamba je, tangu niingie ndoa au utawa, najiona
kumkaribia Mungu Zaidi? Na hili ni swali ambalo watawa wote wakiamka asubuhi na
kabla ya kulala wanapaswa kujiuliza je, maisha yangu ya utawa, au huyu mama
niliyemuoa na familia niliyonayo, je inanisaidia nimkaribie Mungu? Na hili ni
swali ambalo naomba niwaache nalo? Je mimi kwa kusali kwangu jumuiya au kwa
kuja kanisani kunanifanya kweli kumkaribia Mungu. Pale unapoona mambo yakilegea
tuongeze bidii.Tumsifu Yesu Kristo!
Copyright ©2013-2020 ©FurKat,
Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment