Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, NOVEMBA 25, 2021.

 

MASOMO YA MISA, NOVEMBA 25, 2021.

 

ALHAMISI, JUMA LA 34 LA MWAKA WA KANISA

 

SOMO 1.

Danieli 6:12-28

 

Ndipo wakakaribia, wakasema mbele ya mfalme katika habari ya ile marufuku ya mfalme; Je! Hukuitia sahihi ile marufuku, ya kwamba kila mtu atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme, atatupwa katika tundu la simba? Mfalme akajibu, akasema, Neno hili ni kweli, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi isiyoweza kubadilika.

Basi wakajibu, wakasema mbele ya mfalme, Yule Danieli, aliye mmoja wa wana wa wale waliohamishwa wa Yuda, hakujali wewe, Ee mfalme, wala ile marufuku uliyoitia sahihi, bali aomba dua mara tatu kila siku.

Basi mfalme aliposikia maneno haya alikasirika sana, akakaza moyo wake ili kumponya Danieli; akajitaabisha kumwokoa hata jua likachwa.

Ndipo watu wale wakakusanyika pamoja mbele ya mfalme, wakamwambia mfalme, Ee mfalme, ujue ya kuwa ni sheria ya Wamedi na Waajemi, lisibadilike neno lo lote lililo marufuku, wala amri yo yote iliyowekwa na mfalme.

Basi mfalme akatoa amri, nao wakamleta Danieli, wakamtupa katika tundu la simba. Mfalme akanena, akamwambia Danieli, Mungu wako unayemtumikia daima, yeye atakuponya.

Likaletwa jiwe, likawekwa mdomoni mwa lile tundu; naye mfalme akalitia muhuri kwa muhuri yake mwenyewe, na kwa muhuri ya wakuu wake, lisibadilike neno lo lote katika habari za Danieli.

Kisha mfalme akaenda nyumbani kwake, akakesha usiku kucha, akafunga; na vinanda havikuletwa mbele yake; na usingizi wake ukampaa.

Asubuhi mfalme akaondoka mapema, akaenda kwa haraka mpaka penye lile tundu la simba.

Naye alipolikaribia lile tundu, akamlilia Danieli kwa sauti ya huzuni; mfalme akanena; akamwambia Danieli, Ee Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai, je! Mungu wako, unayemtumikia daima, aweza kukuponya na simba hawa?

Ndipo Danieli akamwambia mfalme, Ee mfalme, uishi milele.

Mungu wangu amemtuma malaika wake, naye ameyafumba makanwa ya simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nalionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno.

Basi mfalme akafurahi sana, akaamuru wamtoe Danieli katika lile tundu. Ndipo Danieli akatolewa katika lile tundu, wala dhara lo lote halikuonekana mwilini mwake, kwa sababu alikuwa anamtumaini Mungu wake.

Mfalme akaamuru, nao wakawaleta wale watu waliomshitaki Danieli, wakawatupa katika tundu la simba, wao, na watoto wao, na wake zao; na wale simba wakawashinda wakaivunja mifupa yao vipande vipande, kabla hawajafika chini ya tundu.

Ndipo mfalme Dario akawaandikia watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, waliokaa juu ya uso wa dunia; Amani na iongezeke kwenu.

Mimi naweka amri, ya kwamba katika mamlaka yote ya ufalme wangu watu watetemeke na kuogopa mbele za Mungu wa Danieli; maana yeye ndiye Mungu aliye hai, adumuye milele, na ufalme wake ni ufalme usioharibika, na mamlaka yake itadumu hata mwisho.

Yeye huponya na kuokoa, hutenda ishara na maajabu mbinguni na duniani, ndiye aliyemponya Danieli na nguvu za simba.

Basi Danieli huyo akafanikiwa katika enzi ya Dario, na katika enzi ya Koreshi, Mwajemi.

 

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

 

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 100 (K) Ufu. 19:9

 

(K) Heri walioalikwa karamu ya arusi ya Mwanakondoo.

 

Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote,

Mtumikieni Bwana kwa furaha;

Njoni mbele zake kwa kuimba. (K)

 

Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu;

Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake;

Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake. (K)

 

Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru;

Nyuani mwake kwa kusifu;

Mshukuruni, lihimidini jina lake. (K)

 

Kwa kuwa Bwana ndiye mwema;

Rehema zake ni za milele;

Na uaminifu wake vizazi na vizazi. (K)

 

SHANGILIO

Zab. 25:4 , 5

 

Aleluya, aleluya,

Ee Bwana, unijulishe njia zako, unifundishe mapito yako.

Aleluya.

 

INJILI

Lk. 21:20-28

 

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Hapo mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, ndipo jueni ya kwamba uharibifu wake umekaribia. Ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani, na walio katikati yake wakimbilie nje, na walio katika mashamba wasiuingie. Kwa kuwa siku hizo ndizo za mapitilizo, ili yatimizwe yote yaliyoandikwa. Ole wao wenye miamba na wanaonyonyesha katika siku hizo!

Kwa kuwa kutakuwa na shida katika nchi, na hasira juu ya taifa hili. Wataanguka kwa ukali wa upanga, nao watatekwa nyara na kuchukuliwa katika mataifa yote; na Yerusalemu utakanyagwa na Mataifa, hata majira ya Mataifa yatakapotimia.

Tena, kutakuwa na ishara katika jua; na mwenye, na nyota; na katika nchi dhiki ya mataifa wakishangaa kwa uvumi wa bahari na msukosuko wake; watu wakivunjika mioyo kwa hofu, na kwa kutazama mambo yatakayoupata ulimwengu. Kwa kuwa nguvu z ambinguni zitatikisika. Hapo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika wingu pamoja na nguvu na utukufu mwingi. Basi mambo hayo yaanzapo kutokea, changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia.

 

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristu.

 

 

Copyright © 2020, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment