Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

KUWA WAZALISHAJI KWA AJILI YA UFALME WA MUNGU!

 

“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”

Tafakari ya kila siku

Jumatano, Novemba 17, 2021.

Juma la 33 la Mwaka

 

2 Mak 7: 1, 20-31;

Zab 17: 1, 5-6, 8, 15 (K) 15;

Lk 19: 11-28.

 

 

 

KUWA WAZALISHAJI KWA AJILI YA UFALME WA MUNGU!

 

Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana linazidi kutupa habari juu ya mashahidi wake, jinsi walivyokuwa tayari hata kuutoa uhai wao, wapate kumtukuza Mwenyezi Mungu.

 

Somo la kwanza mfalme Antiokus anaendelea kuwatesa Wayahudi akiwataka waiache imani yao na tamaduni zao takatifu. Mfalme huyu anakuwa hata tayari kuwahonga baadhi ya Wayahudi ili ati waziache desturi zao na kufuata desturi za kipagani. Lakini vijana wa leo pamoja na mama yao wanatambua hasara itakayosababishwa na kitendo chao cha kupokea rushwa ya mfalme na hivyo kuvunja desturi zao hadharani. Walijua kwamba kitendo kile kitawakatisha tamaa waliowengi na kuzifanya desturi za kiyahudi kupoteza nguvu kwa haraka. Hivyo waliamua kuchagua kifo na kile kifo chao na uaminifu wao ulizisaidia desturi za kiyahudi kuendelea kupata heshima.

 

Ndugu zangu, vijana wa somo la kwanza wanakuwa kwetu mfano kwa siku ya leo-kwamba mambo ya Mungu, mambo ya imani ni ya thamani kubwa. Hayapaswi kufanyiwa mzaha kama mfalme Antiokus alivyotaka kuidanganya familia ya leo, au kama walivyotaka kumdanganya mzee Eleazar katika somo tulilolisikia jana. Hatupaswi kuwa tayari kupokea rushwa ili tulegeze sheria na miiko ya imani yetu. Yapo baadhi ya maeneo ambapo kanisa limekosa nguvu ya kinabii baada ya baadhi ya viongozi wao kukubali kushawishiwa kirahisi na kupokea rushwa fulani. Hivyo waamini wengi wamekatishwa tamaa na kuiona dini kama utapeli, inayotumiwa na viongozi kuwatapeli watu.Tujifunze kuogopa rushwa katika kanisa.

 

Katika somo la injili, Bwana Yesu anatoa mfano kuhusu ufalme wa mbinguni na wajibu wa mwanadamu katika ufalme huo. Mungu anafananishwa na mfalme aliyewapatia raia wake talanta mbalimbali na baadaye atataka hesabu kwao. Ukweli ni kwamba waliopewa kingi walizalisha kingi lakini waliopewa kidogo walizalisha kidogo. Tulitegemea labda ingetokea kwamba aliyepewa kidogo azalishe kingi kuliko aliyepewa kingi lakini ni yule tu aliyepewa kingi ndiye aliyezalisha kingi.

 

Kwa hakika Mungu hutoa kuendana na uwezo wetu, hekima yetu, na ukomavu wetu. Wapo ambao kama wangalipewa vingi na Mungu wangaliishia kuharibu na kuonesha uzembe na hivyo kuzifanya rasilimali za Mungu zipoteee. Mungu hutoa kwa kadiri yule aliyekabidhiwa anavyoonesha ushirikiano naye. Wapo waliowahi kupewa na mwishowe kunyanganywa kwa sababu ya kuonesha uvivu, uzembe, na kukosa ukomavu. Neno hili litutie moyo na kutuhamasisha ili tuweze kuwa washiriki hodari pamoja na Mwenyezi Mungu.

 

Tushirikiane naye, tumwombe kila siku atusaidie kutumia vyema kile alichotupa ili kisije kikapotea au kutupwa bure.

Copyright ©2013-2020 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

 

No comments:

Post a Comment