ASALI
ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari
ya kila siku
Jumanne,
Novemba 23, 2021
Juma
la 34 la Mwaka wa Kanisa
Dan
2: 31-45;
Dan
3: 57-61 (K) 59;
Lk
21: 5-11.
KUJIANDAA
KWA MWISHO WA ULIMWENGU
Karibuni
sana wapendwa wa Bwana kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Katika
somo la kwanza leo, Danieli anamfafanulia mfalme Nebuchadneza ndoto ya ajabu
aliyoiona. Ndoto hii aliona sanamu kubwa, nzuri, iliyosifika sana. Ilikuwa
imeundwa kwa fito za thamani na kwa hakika iliweza kutambulika na wengi. Lakini
cha ajabu sanamu hii ilivunjwa vipande vipande kwa jiwe la ajabu lisilo kazi ya
mikono ya mwanadamu lilipiga sanamu hii na kuivunja vipande vipande. Nafasi ya
sanamu hii ilipotea.
Mwangavu
wake na umaarufu wake na sifa zake zilipotea. Sanamu hii ni maono na ishara
zenye kuashiria ujio wa nyakati za mwisho. Ni kiashirio cha falme na tawala
zitakazoitawala dunia. Mwishowe tawala hizi zitaondoshwa zote. Atakayetawala ni
Mungu mwenyewe. Ndio utawala utakaobakia milele. Ndio utawala wenye kuvunja
vunja tawala nyingine za dunia.
Sisi
tujifunze kumtumikia mwenyezi Mungu tuwapo hapa dunia. Tunaofanya kazi katika
serikali na taasisi mbalimbali tujitahidi ili taasisi hizo ziishi kwa ajili ya
Bwana na zimtumikie Bwana. Zisiendeleze uovu kwani tawala zote zilizo ovu
zitashindwa mwishowe.
Tujitahidi
kufanya mema. Tusiungane na wakorofi ili kukandamiza walio wadogo. Kila
tulichonacho kimtumikie Bwana na kimfanye Bwana atawale.
Yesu
katika injili anazidi kuelezea tena kuhusu nyakati za mwisho. Anazungumza kwa
kulitolea mfano hekalu kwamba japokuwa lapendeza na kuwa na vitu vya thamani,
kwa hakika itakuja siku moja vitu vyote hivyo vitaharibiwa. Dhahabu na vyote
vilivyomo vitaachwa.
Kwa
hakika Yesu alitumia mfano huu kuonesha kwamba mambo yote yatakuwa na mwisho,
hata yale mazuri tunayoyajenga. Hivyo tujifunze kuthamini yaliyo ya Mungu
kuliko yote. Tuache tabia ya kujitumikia sisi wenyewe tu. Pia tuwe makini
tusirubuniwe na matapeli mbalimbali. Tujifunze kumtumikia Mwenyezi Mungu siku
zote.
Tujiepushe
kuwa watu wa tamaa na hivyo kufuata kirahisi maelezo ya matapeli. Tamaa zetu za
kupenda mambo marahisi rahisi hutufanya tukamatwe kirahisi na matapeli. Tambua
kila kitu ulichonancho kiwe kizuri namna gani, nyakati zitafika kila kitu
kitabomolewa na kuondoshwa kitakacho baki cha maana ni imani yako kwa Bwana.
Ilinde usiipoteze.
Copyright ©2013-2020 ©FurKat,
Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment