“ASALI
ITOKAYO MWAMBANI”
Jumanne,
Novemba 9, 2021
Juma
la 32 la mwaka wa Kanisa
Sikukuu
ya Kutabarukiwa kwa Basilika la Laterani
Ez
47:1-2, 8-9, 12;
Zab
45:2-3, 5-6, 8-9;
1Kor
3: 9-11, 16-17;
Yn
2:13-22
HEKALU
LA MUNGU!
Karibuni
ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo tunaadhimisha
sikukuu ya kutabarukiwa kanisa la Laterano. Hili ni kanisa kuu la jimbo la
Roma. Ndilo kanisa kongwe kwa upande wa wakristo wa magharibi; na lilijengwa na
mfalme Constantino na mwanzoni kila aliyetaka kuwa mkristo ilibidi abatiziwe
ndani ya hili kanisa na lilitabarukiwa na Papa Sylvester mwaka 324.
Hili
huonekana kama kanisa mama na kuadhimisha sherehe yake kutabaruku ni ishara ya
muungano wa makanisa yote chini ya kanisa moja na uongozi mmoja. Sherehe hii
twasherekea ukuu wa Mungu wa kusimika jamii ya kiimani ndani ya ulimwengu huu,
ni ishara wa uwepo wa jamaa ya Kikristo inayomwabudu Mungu wakati wote popote
duniani. Sisi ni sehemu ya jamaa hii na hivyo lazima tuwe jamii yenye uhai,
tusilegelege.
Siku
ya leo masomo yetu ya leo yanatuongoza kutafakari sikuu ya leo. Zaburi ya leo
ya wimbo wa katikati inazungumzia juu ya uwepo wa mto unaoupatia furaha mji
ambapo Mungu ameweka makao yake. Huu mto ni neema za Mungu ambazo uwepo wake ni
sababu ya mji huo kubarikiwa.
Mto
huu katika somo la kwanza unaonyeshwa ukitoka katika hekalu la Mungu na kila
maji yake yanapopitia panapata uhai na kuneemeka. Yote haya ni kutokana na
nguvu za Mungu. Unabii huu wa Ezekieli katika somo la kwanza uliwahusu wana wa
Yuda ambao kwa kipindi kirefu walitenda dhambi wakafukuza utukufu wa Mungu
ndani ya lile hekulu.
Ukisoma
sura ya 11 ya kitabu cha Ezekiel tunaanza kuona jinsi alivyoanza kuondoka
hekaluni. Kitendo cha Mungu kutoka hekaluni, lile hekalu lilikosa nguvu na mji
wote ukakosa nguvu na kusababisha kuangamizwa na Wababuloni. Kulitokea laana na
shida.
Leo
basi Mungu anarudi hekaluni na hakika kunakuwa tena neema. Na anadhihirisha
kwamba kwa yeyote anayeshirikiana naye, popote pale walipo watabarikwa zaidi.
Hekalu
letu ni kanisa letu ndugu zangu. Ndicho chanzo cha neema. Neema hizi tunazipata
tukiwa katika muunganiko na kanisa, chini ya kiongozi mmoja Yesu Kristo
anayewakilishwa na Papa kwa hapa duniani. Tuwe katika muunganiko na Kanisa tuzipate
neema hizi, tukiwa mbali na kanisa ni chanzo cha sisi kukosa ulinzi na kubomoka
kama ule mji wa Yerusalemu ulivyobomolewa na wababuloni kwa sababu Mungu
alikosekana ndani yake. Walikosa ulinzi wa Mungu.
Yesu
katika injili anadhihirisha kwamba hekalu lake ni nyumba ya sala na neema.
Iheshimiwe na kutunzwa. Nasi tuyatunze makanisa yetu. Tusifanyie hapo biashara
au harambee kiasi cha kuonekana kuwa nyumba ya biashara. Iwe sehemu ya kupatia
neema.
Ukipewa
nafasi ya kudeki kanisa usipige kelele tena kupiga michapo ndani ya kanisa,
hata wakati mwingine kumsengenyea mtu ndani ya kanisa. Kanisa ni sehemu
takatifu, usipatumie kutegesha mitego yako, kutafutia hapo mwanaume mzuri, au
mwanamke mzuri, au unatembea bila heshima nk. Sehemu takatifu ni sehemu bora kuliko
sehemu yeyote duniani.
Copyright ©2013-2020 ©FurKat,
Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment