Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

FUATA NA ONGOZA!

 

“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”

Jumanne, Novemba 30, 2021

Juma la 1 la Majilio

 

Sikukuu ya Mt. Andrea Mtume,

 

Rum 10: 9-18;

Zab 19: 2-5 (R. 5);

Mt 4: 18-22.

 

 

FUATA NA ONGOZA!

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu. Leo tunaadhimisha sikukuu ya mtume Adrea. Yeye alikuwa nduguye na Simon Petro na wote ni wenyeji wa Betsaida. Mtume huyu alihubiri sana huko barani Asia hasa katika maeneo ya Ugiriki na Costantinople. Alikufa kishahidi kwa kusulubiwa juu ya msalaba wenye sura ya X huko katika mji wa Patras, katika jimbo la Achaea Ugiriki.

 

Katika somo la kwanza, tunasikia mtume Paulo akielezea juu ya faida ya kumtambua na kumwamini Yesu na hivyo anasisitiza watu wajitokeze ili huyo Kristo apate kuhubiriwa na kuaminiwa na wengi.

 

Katika Injili, tunasikia kwamba kumhubiri Kristo ni kuwa mvuvi wa watu, yaani kuziokoa roho za watu katika dunia ambayo ni kama bahari inayosukumwa na mawimbi mbalimbali ambayo kama hajajitokeza mtu wa kuwaokoa watu, watu wote wanazama, roho zote zinakunywa maji. Lakini ili uweze kuzivua hizi roho ili zisisombwe na mavimbi, yabidi wewe uwe na maarifa Zaidi, ujue kuogelea na uwe na vifaa maalumu kwa kazi hii. *Imani na tabia njema* za hawa mitume ndizo zilizowasaidia mitume kama akina Andrea kuweza kuwaokoa Wakristo katika mitego yote ya muovu. Kwa nanma hii waliweza kumpatia Kristo utukufu na hata kukubali kufa kifo shahidi.

 

Mtume Andrea alikuwa mvuvi. Moja ya tabia za wavuvi kipindi hicho ni kwamba hawa walikuwa washirikina. Waliweza kubadilika baada ya kukutana na Yesu. Lakini taratibu taratibu waliweza kufanya bidii na kuweza kuziokoa roho za ukristo zisisombwe na ushirikina. Nasi ndugu zangu tusikatishwe tamaa na historia zetu. Yawezekana huko nyuma tulishawahi kufanya mambo mabaya tukawa wadhambi sana. Lakini sasa tukimtumainia Kristo nakwambia tutafika mbali Zaidi na hata tutaweza kuja kuwa watakatifu.

 

Kingine ni kwamba, Mkristo yeyote lazima awe na kitu amevua kwa siku au mwaka mzima; kuwakomboa watu kutoka utawala wa kishetani. Yesu anataka utawala wa shetani ushindwe. Angalia isije ikawa kwamba wewe kazi yako ni kuwazamisha samaki katika dhoruba Zaidi. Kwa matendo yetu mabaya kama ulevi, uasherati, nyumba ndogo, masengenyo na umbea hutufanya tuzizamishe roho za watu badala ya kuzivua.

 

Unaposali na kutenda matendo mema, hivi huwa kama chambo zinazozivutia samaki na kwa namna hii utaweza kuwavua samaki wengi, kuziokoa roho za watu.

 

Utume wa kuhubiri injili ni utume mkubwa sana kwa sababu huhusika na roho za watu na hivyo wahitaji uchukuliwe kwa umakini mkubwa. Hivyo, yeyote anayedili na utume huu atambue thamani yake na kujitoa ipasavyo kuziokoa hizi roho. Waite watu watubu, waache matendo machafu na kumrudia Mungu.

 

Copyright ©2013-2020 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

 

No comments:

Post a Comment