Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

UWE IMARA NA TAMBUA MIMI NI MUNGU!

 

“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”

Tafakari ya kila siku

Jumanne, Oktoba 5, 2021,

Juma la 27 la Mwaka

 

Yon 3: 1-10

Zab 130: 1-4, 7-8 (K) 3;

Lk 10: 38-42.

 

 

UWE IMARA NA TAMBUA MIMI NI MUNGU!

 

 

Karibuni ndugu zangu katika adhimisho la Ekaristi takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika asubuhi ya leo tunaaanza kwa kuliangalia somo la kwanza toka katika kitabu cha Nabii Yona. Hapa tunamkuta Yona akihubiri toba kwa watu wa Ninawi na watu wa ninawi wanaipokea kwa moyo mmoja na mara moja toba inaanza na Mungu anawasamehe.

 

Sehemu hii ya Biblia ni miongoni mwa maeneo machache ambapo nabii ameongea na kusikilizwa mara moja. Mara nyingi nabii alipoongea-walimuona kama kichaa, kachanganyikiwa vile-hivyo hawakumsikiliza hata kidogo-sehemu nyingine walichapwa viboko au kufungwa gerezani au kupigwa na mawe. Lakini hapa ni ajabu kabisa. Watu wameitikia wito mara moja.

 

Tujiulize ni kwa nini? Ni kwa sababu watu wa Ninawi hawakuwa watu wa taifa moja na Yona. Hawakuwa Wayahudi-nabii hakubaliki katika nyumba yake-watu hawa waliuchukulia ujumbe huu kwa makini sana na Mungu anapenda watu wa namna hii na ndiyo maana anawaondolea adhabu yao.

 

Katika injili, Yesu anaonesha tena dhahiri kwamba Yesu anawapenda watu wanaouchukulia ujumbe wa Mungu kwa makini-hawa ni akina Maria-unakaa mguuni mwa Yesu-unauelewa kwanza ule ujumbe halafu ndio ukautoe kwa watu ukiwa na uelewa tosha. Tofauti na Martha-yeye alikuwa anapilikapilika tu muda wote-sasa angepata muda upi wa kuuelewa ujumbe wa Mungu. Na kama hajaulewa atapeleka nini kwa watu, atatumikiaje watu?

 

Hivyo sote kama Maria lazima tukae kwa Yesu atufunze kwanza halafu ndio tuende tukahudumie watu. Huwezi kuhudumia bila kuwa na uelewa wa kile unachohudumu.

 

Somo hili linawagusa sana hasa watu wanafunzi, au watu wote wanaojidai kuwa bize masaa 24 bila kuwa na muda wa kukaa kwa Yesu. Mwisho wa siku wanashindwa kuelewa maana ya kile wanachofanya-wanakata tamaa kwa haraka kwa sababu hukumshirikisha Mungu. Utaamka asubuhi kwenda kusoma lakini kama hujakaa miguuni pa Yesu-nakwambia unajihangaisha tu.

 

Kaa miguuni pa Yesu kama Maria. Utakaanga chips na vitumbua kila siku lakini utasema kuna shetani ananiibia fedha, utauza duka lakini ukipiga faida huoni-mwishoni utasema kuna shetani linaniibia fedha. Au kama ni mwanafunzi utasema kuna mtu ananiibia hizi akili zangu au kuna mtu anatuma jini lake na kuja kufyonza akili zangu na kuzimpatia yeye ninapokuwa nimelala. Kumbe sababu ni kwamba hukai miguuni kwa Yesu na kusikiliza neno lake. Tusiwe wachoyo wa kutafuta muda wa kukaa na Yesu.

 

Copyright ©2013-2021 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment