MASOMO YA MISA, OCTOBER 5, 2021
JUMANNE, JUMA LA 27 LA MWAKA
SOMO 1
Yon. 3:1-10
Neno la Bwana likamjia Yona mara ya
pili, kusema, Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa, ukaihubiri habari
nitakayokuamuru. Basi Yona akaondoka, akaenda Ninawi, kama Bwana alivyonena.
Basi Ninawi ulikuwa mji mkubwa mno, ukubwa wake mwendo wa siku tatu. Yona
akaanza kuuingia mji mwendo wa siku moja, akapaza sauti yake, akasema, Baada ya
siku arobaini Ninawi utaangamizwa.
Basi watu wa Ninawi wakamsadiki, Mungu;
wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za magunia, tangu yeye aliye mkubwa hata
aliye mdogo. Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti
chake cha enzi, akavua vazi lake, akajivika nguo za magunia, na kuketi katika
majivu. Naye akapiga mbiu, akatangaza habari katika mji wa Ninawi, kwa amri ya
mfalme na wakuu wake; kusema, Mwanadamu aisonje kitu, wala mnyama wala makundi
ya ng’ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji; bali na
wafunikwe nguo za magunia, mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie Mungu kwa
nguvu, naam, na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio
mikononi mwake. Ni nani ajuaye kwamba Mungu hatageuka na kughairi, na kuiacha
hasira yake kali, ili tusiangamizwe? Mungu akaona matendo yao, ya kuwa
wameiacha njia yao mbaya.
Basi Mungu akalighairi neno lile baya,
ambalo alisema atawatenda; asilitende.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 130:1-4.7-8
(K) Bwana, kama Wewe ungehesabu maovu,
nani angesimama?
Ee Bwana, toka vilindini nimekulilia.
Bwana uisikie sauti yangu.
Masikio yako na yaisikilize
Sauti ya dua zangu. (K)
Bwana, kama Wewe ungehesabu maovu,
Ee Bwana, nani angesimama?
Lakini kwako kuna msamaha,
Ili Wewe uogopwe. (K)
Ee Israeli, umtarajie Bwana;
Maana kwa Bwana kuna fadhili,
Na kwake kuna ukombozi mwingi.
Yeye atamkomboa Israeli na maovu yake
yote. (K)
SHANGILIO
Efe. 1:17,18
Aleluya, aleluya,
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, awape
roho ya hekima, mjue tumaini ya mwito wake.
Aleluya.
INJILI
Lk. 10:38-42
Yesu aliingia katika kijiji kimoja;
mwanamke mmoja jina lake Martha akamkaribisha nyumbani kwake. Naye alikuwa na
umbu lake aitwaye Mariamu, aliyeketi miguuni pake Yesu, akasikiliza maneno
yake. Lakini Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi; akamwendea,
akasema, Bwana, huoni vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke
yangu? Basi mwambie anisaidie.
Bwana akajibu akamwambia, Martha,
Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi; lakini kinatakiwa
kitu kimoja tu; na Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristu.
Copyright © 2020, "MASOMO YA
MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings
reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment