“ASALI
ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari
ya kila siku
Jumamosi,
Oktoba 23, 2021
Juma
la 29 la Mwaka
Warumi 8:1-11
Zaburi 24:1-2.3-4ab.5-6 (R. see 6)
Luka 13:1-9
TUMITWA
TUWE WAKAMILIFU!
Ndugu zangu wapendwa karibuni kwa
adhimisho la Ekaristi Takatifu asubuhi ya leo. Katika somo la kwanza tunaona
Paulo akiendelea kuwaasa Warumi kuhusu madhara ya kufuata vionjo vya mwili,
mwili daima hupeleka mtu kwenye mauti kama utaufuata kwa kila kitu
unachohitaji. Wakati roho inakuambia bia moja inatosha mwili unasema ongeza
nyingine, mwili unataka ule tuu chakula na unatamani hata vitu vyenye sukari
nyingi bila hata kujali kwamba ni madhara kwake wenyewe lakini ukitii hakika
mwisho lazima mauti yaje haraka. Mwili unakusukuma nenda nje ya ndoa yako,
haukutakii mema utapatwa na magonjwa na mwisho ni mauti.
Leo Paulo anatuasa nasi tusitumikie
mwili bali tufuate sheria ya Kristo inayoongozwa na roho katika dhamiri safi.
Kwa namna hiyo tutapata uzima na hatutakumbwa na mauti ya milele.
Ndugu zangu tujifunze kuwa na kiasi
katika kuuthibiti mwili, kuuongoza na sio kuutii daima, kula kwa kiasi, kunywa
kwa kiasi. Usile kila kitu, kuwa na muda wa kula pia usile hofyo hofyo
nakunenepa nakupatwa na magonjwa. Tusiwe watumwa wa pombe, tusishindane na
kiwanda cha bia. Usiwe mtumwa wa sigara nakupeleka mwili wako kwenye mauti.
Katika somo la injili Yesu anatoa mfano
wa walioangukiwa na mnara na kufa kifo kibaya na kufundisha kwamba haimaanishi
hawa wanaopatwa na mkasa huu ndio wadhambi.
Wakati mwingine sisi tunaobaki ndio
wadhambi zaidi. Kile kipindi cha sisi tunabakia bila kuadhibiwa na tunabakia
kusikia na kuona maumivu ya wengine ni kipindi cha kutufunza ili tuache dhambi.
Ajali za wengine na mateso yao unayaona kwenye tv, au wakimbizi wakilia yote
haya ni nafasi zitutakazo tuongeze bidii tuweka samadi ya kiroho. Ni kipindi
ambacho tunatiliwa samadi kama huyu mkulima anavyofanya kwa huu mti wake ili
tubadilike na tusipobadilika tutakatwa.
Wadhambi wengi tunaendelea kuishi kwa
sababu ya huruma ya Mungu. Kati yetu tunaishi na watu ambao labda tungaliomba
wawe wamekwishaadhibiwa tayari lakini Yesu anaruhusu waendelee kuishi ili basi
wabadilike, ni huruma ya mkulima. Sisi tubadilike na tukiona hatujaadhibiwa
tusijione ati sisi ni wajanja sana au Mungu hana nguvu. Mungu akiamua,
nakueleza sisi hatutasalia. Tuombe kutumia nafasi tupewazo vyema. Wengi
tunatumia vibaya kile kipindi Mungu anapokaa kimya na kuamua kumtukana na
kumwona kana kwamba hana nguvu. Kwa hapa tunajilaani zaidi. Mungu ni mkuu kila
wakati. Tuache kumkosea adabu.
Copyright ©2013-2021 ©FurKat, Furaha ya
Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
No comments:
Post a Comment