Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, JUMAMOSI, 23, 2021

 MASOMO YA MISA, JUMAMOSI, 23, 2021

 JUMAMOSI JUMA LA 29 LA MWAKA

 

SOMO 1.

Warumi 8:1-11

 

Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu.

Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti.

Maana yale yasiyowezekana kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa dhaifu kwa sababu ya mwili, Mungu, kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa sababu ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili;

ili maagizo ya torati yatimizwe ndani yetu sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya roho.

Kwa maana wale waufuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili; bali wale waifuatao roho huyafikiri mambo ya roho.

Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti; bali nia ya roho ni uzima na amani.

Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii.

Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu.

Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake.

Na Kristo akiwa ndani yenu, mwili wenu umekufa kwa sababu ya dhambi; bali roho yenu i hai, kwa sababu ya haki.

Lakini, ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu.

 

Neno la Bwana......Tumshukuru Mungu.

 

WIMBO WA KATIKATI.

Zaburi 24:1-2.3-4ab.5-6 (R. see 6)

 

(K)Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao,

 

Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya BWANA,

Dunia na wote wakaao ndani yake.

Maana ameiweka misingi yake juu ya bahari,

Na juu ya mito ya maji aliithibitisha.

(K)

 

Ni nani atakayepanda katika mlima wa BWANA?

Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake?

Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe,

Asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili,

(K)

 

Atapokea baraka kwa BWANA,

Na haki kwa Mungu wa wokovu wake.

Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao,

Wakutafutao uso wako, Ee Mungu wa Yakobo.

(K)

 

SHANGILIO.

Ezekieli 33:11

 

Aleluia Aleluia!!

sikufurahii kufa kwake mtu mwovu; bali aghairi mtu mwovu, na kuiacha njia yake mbaya, akaishi.

Aleluia!!

 

INJILI.

Luka 13:1-9

 

Na wakati uo huo walikuwapo watu waliompasha habari ya Wagalilaya wale ambao Pilato alichanganya damu yao na dhabihu zao.

Akawajibu akawaambia, Je! Mwadhani ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na mambo hayo?

Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.

Au wale kumi na wanane, walioangukiwa na mnara huko Siloamu, ukawaua, mwadhani ya kwamba wao walikuwa wakosaji kuliko watu wote waliokaa Yerusalemu?

Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.

Akanena mfano huu; Mtu mmoja alikuwa na mtini umepandwa katika shamba lake la mizabibu; akaenda akitafuta matunda juu yake, asipate.

Akamwambia mtunzaji wa shamba la mizabibu, Tazama, miaka mitatu hii naja nikitafuta matunda juu ya mtini huu, nisipate kitu; uukate, mbona hata nchi unaiharibu?

Akajibu akamwambia, Bwana, uuache mwaka huu nao, hata niupalilie, niutilie samadi;

nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo uukate.

 

Neno la Bwana......Sifa kwako ee kristo.

 

Copyright © 2020, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment