“ASALI
ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari
ya kila siku
Jumamosi,
Oktoba 2, 2021.
Juma
la 26 la Mwaka
Kumbukumbu
ya Malaika Walinzi
Kut
23: 20-23;
Zab
90: 1-6, 10-11;
Mt
18: 1-5, 10
MALAIKA
–ULINZI WA MUNGU KWETU
Karibuni
ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo basi
tunaadhimisha kumbukumbu kwa ajili ya malaika walinzi; malaika wanaotembea nasi
wakitulinda kila wakati. Uwepo wa malaika huyu ni alama kubwa sana ya upendo
inayodhihirisha kwamba kweli Mungu anatupenda sana; katuwekea malaika
anayeangalia kila hatua tunayofanya. Hili linapaswa kutufurahisha.
Lakini
cha ajabu ni kwamba hili limewakasirisha wengi, wengi tumeona kana kwamba uwepo
wa huyu malaika kama ati Mungu anazidisha kutufuatilia, hatupatii uhuru, hivyo
basi wengi wetu tumemfukuza-na huyu malaika akishakaa pembeni, huo ndio mwanzo
wa maanguko wa maisha ya mwanadamu kwani yeye hubakia bila mlinzi na shetani
hutukamata kirahisi. Huyu ndiye malaika mlinzi.
Masomo
yetu leo tena yanatukaribisha vyema kwenye kuuona ukuu wa malaika huyu. Mzaburi
katika wimbo wa katikati anatueleza jinsi Mungu alivyomuweka huyu malaika
akielewa kila tunachofanya, na jinsi Mungu asivyopenda njia yetu hata moja
ishindwe kutuongoza mbele kwa Mungu.
Somo
la kwanza linatuonesha jinsi Mungu alivyowapatia malaika wa namna hii wana wa
Israeli walipokuwa kule jangwani ili awawezeshe kupita ndani ya lile jangwa.
Lile jangwa lilikuwa ni jangwa baya sana. Lilijaa nyoka wa sumu, makabila yenye
hasira, na ukame mwingi sana. Hivyo walihitaji wa kuwaongoza ili wawaepe hawa
maadui na kweli malaika mlinzi alifanya kazi hii vyema. Pale waliposhirikiana
na huyu malaika, kweli walifaulu, walipata chakula, hawakushambuliwa na kabila
lolote na hakuna nyoka aliyewadhuru.
Lakini
walipoonesha ukaidi, walijikuta wakikumbana na nyoka tena wenye sumu, makabila
yenye hasira, na ukame wa hali ya juu na kiu.
Yesu
katika Injili anatuambia kwamba bado tunaye malaika wa namna hii kwa kila
mmoja. Hivyo tumtegemee huyu malaika. Tumwalike, atuepushe na nyoka wa sumu wa
hapa dunia, atuoneshe tukanyage wapi, atuepushe na ajali mbalimbali. Bila huyu
malaika tutadumbukia kwenye mitego mingi sana ya shetani ya ulimwengu.
Wengi
tumedumbukia kwenye mitego ya uasherati, hasira, ulevi na tamaa kwa sababu ya
kumtupa pembeni huyu malaika. Na kubakia bila mlinzi-hii ni hatari sana-kubakia
bila mlinzi.
Tusikubali
kubakia bila huyu malaika kwani kwa hakika tutapeperushwa kirahisi na shetani.
Kingine
tutambue kama injili inavyotueleza kwa siku ya leo kwamba tusimuonee yeyote
aliyemdogo kwa sababu ya uwepo wa malaika wanaowalinda watu kama hawa. Waweza
kutumia nguvu nyingi kutaka kudhulumu aliyemdogo lakini bado tukashindwa. Yeye
akianguka magotini kwa Bwana na kupata ulinzi wa huyu malaika, hakika
hutamshinda. Na zaidi tutapata laana. Tusiwaonee wadogo ili tusije tukapata
laana za kuadhibiwa na huyu malaika.
Pia
tushirikiane naye kama Mwenyezi Mungu anavyowaeleza wana wa Israeli leo. Wengi
tunakosa ushirika naye na ndio maana tunaanguka kirahisi katika mitego ya
shetani. Na pale tunapotenda dhambi, huwa tunamkufuru kwani yeye yupo na dhambi
zetu zinasababisha ukuta kati yetu na yeye. Tukimbie dhambi ndugu ili malaika
wetu awe karibu nasi zaidi. Tumsifu Yesu Kristo.
------------------------
Copyright ©2013-2020
©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment