“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Jumatatu, Septemba 13,
2021,
Juma la 24 la Mwaka
1 Tim 2:1-8
Zab 28: 2, 7-9
Lk 7: 1-10.
SISTAHILI!
Karibuni sana ndugu
wapendwa kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika
somo la kwanza, Paulo anamweleza Timotheo kwamba anataka dua na sala na
maombezi na shukrani zifanyike kwa ajili ya watu wote, wafalme, na wote wenye
mamlaka, tuishi maisha ya utulivu na amani, katika utauwa wote na ustahilivu.
Maombi haya tunaomba na
sisi tuyapokee siku ya leo na kuyatumia. Tuwaombee viongozi wetu na wote wenye
mamlaka. Hakika wanahitaji waombewe afya njema na nguvu kwa sababu wapo wenye
wajibu mzito. Wapo ambao kila siku lazima wahudhurie mkutano zaidi ya mmoja,
ratiba zao zimebana ajabu. Wapo ambao wanapaswa kufanya maamuzi ambayo endapo
watakosea kidogo au kutokutumia hekima, yaweza kuleta madhara mengi kwa jamii.
Baadhi ya mikataba wanayopaswa kusign ni ya muhimu kiasi kwamba wakikosea
kidogo, wataitumbukiza jamii katika matatizo makubwa.
Pia upo wakati
wanapokumbana na vikwazo toka katika mataifa makubwa vikiwataka wakubaliane na
vikwazo vyao mbalimbali. Sisi tunapaswa kuwaombea viongozi wetu hawa wawe na
hekima pale wakumbanapo na ugumu wa namna hii. Tujiombee na sisi wenyewe ili
tuweze kuwa na hekima ya kuamua na kutulia pale tukumbanapo na mazingira magumu
yatuhitajiyo kufanya uamuzi mzito.
Katika somo la injili,
Yesu anaonesha furaha yake baada ya kwenda kumponya mgonjwa wa mtu mwenye
imani. Yesu ametiwa moyo na familia ya Akida kwa sababu ni familia yenye imani;
kwanza inamheshimu Yesu na kumpatia nafasi yake, halafu inajua ni namna gani
impokee. Na hili linamfanya Yesu atiwe moyo na kupata furaha mbele ya umati
wote mkubwa.
Sisi tutambue kwamba kwa
matendo yetu ya imani, tunamfanya Yesu afurahi na kupata heshima. Tusichoke
kumpatia Yesu heshima kwa imani yetu. Miongoni mwa eneo ambapo tunapaswa
kumpatia Yesu heshima ni katika Ekaristi takatifu. Imani yetu haba inamfanya
adharaulike katika Ekaristi. Tuongeze imani kwa ekaristi, tumkiri Yesu wa
Ekaristi kama huyu akida anavyofanya leo kila tuipokeapo.
------------------------
Copyright ©2013-2020
©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment