Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, JUMATATU, SEPTEMBA 13, 2021

 

MASOMO YA MISA,

JUMATATU, SEPTEMBA 13, 2021

JUMA LA 24 LA MWAKA

 

SOMO I

1 Tim 2: 1-8

 

Kabla ya mambo yote, nataka dua, na sala, na maombezi, na shukrani, zifanyike kwa ajili ya watu wote; kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, tuishi maisha ya utulivu na amani, katika utauwa wote na ustahivu. Hili ni zuri, nalo lakubalika mbele za Mungu Mwokozi wetu, ambaye hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli. Kwa sababu, Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na mwanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu, ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote, utakaoshuhudiwa kwa majira yake. Nami kwa ajili ya huo naliwekwa niwe mhubiri na mtume, (nasema kweli, sisemi uongo), mwalimu wa Mataifa katika imani na kweli. Basi, nataka wanaume wasalishe kila mahali, huku wakiinua mikono iliyotakata pasipo hasira wala majadiliano.

 

Neno la Bwana...Tumshukuru Mungu

 

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 28: 2, 7-9

 

(K.) Na ahimidiwe Bwana,

maana ameisikia sauti ya dua yangu.

 

Uisikie sauti ya dua yangu

nikuombapo,

nikipainulia mikono yangu

patakatifu pako. (K.)

 

Bwana ni nguvu zangu na ngao yangu

moyo wangu umemtumaini

nami nimesaidiwa; basi, moyo wangu unashangilia,

na kwa wimbo wangu nitamshukuru. (K.)

 

Bwana ni nguvu za watu wake,

naye ni ngome ya wokuvu kwa masiya wake.

Uwaokoe watu wako, uubariki urithi wako,

Uwachunge, uwachukue mileke. (K.)

 

SHANGILIO

Yn. 3: 16

 

Aleluya, aleluya,

Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu,

hata akamtoa Mwanawe pekee,

ili kila mtu amwaminiye asipotee,

bali awe na uzima wa milele.

Aleluya.

 

INJILI

Lk. 7: 1-10

 

Yesu alipokwisha kuyamaliza maneno yake yote masikioni kwa watu, aliingia Kapernaumu. Na mtumwa wake akida mmoja alikuwa hawezi, karibu na kufa; naye ni mtu aliyempenda sana. Aliposikia habari za Yesu, alituma wazee wa Wayahudi kwake kumwomba aje amponye mtumwa wake. Nao walipofika kwa Yesu, walimsihi sana wakisema, Amestahili huyu umtendee neno hili; maana, analipenda taifa letu, naye alitujengea sinagogi. Basi Yesu akaenda pamoja nao.

 

Hata alipokuwa si mbali na nyumba yake, yule akida alituma rafiki kwake, akamwambia, Bwana, usijisumbue, maana mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu; kwa hiyo nilijiona sistahili mwenyewe kuja kwako; lakini, sema neno tu, na mtumwa wangu atapona. Kwa maana mimi nami ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu, Nenda, huenda; na huyu, Njoo, huja; na mtumwa wangu, Fanya hivi, kufanya. Yesu aliposikia hayo alimstaajabia, akaugeukia mkutano uliokuwa ukimfuata, akasema, Nawaambia, hata katika Israeli sijaona Imani kubwa namna hii. Na wale waliotumwa waliporudi nyumbani, wakamkuta yule mtumwa ni mzima.

 

Neno la Bwana...Sifa kwako, ee Kristo

-------------------------

Copyright © 2020, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment