“ASALI
ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari
ya kila siku
Jumamosi,
Septemba 25, 2021.
Juma
la 25 la Mwaka
Zek
2: 5-9, 14-15;
Yer
31: 10-12, 13;
Lk
9: 43-45
ROHO
MTAKATIFU ANAFUMBUA MAFUMBO YA IMANI!
Ndugu
zangu wapendwa, karibuni kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la
Bwana katika somo la kwanza Nabii Zekaria anaelezea juu ya utukufu utakaolipata
taifa la Israeli. Anatangaza kuja na kukaa kati yao na mataifa mengi yataujia
mji wa Yerusalemu na kuupatia utukufu. Na Bwana atakuwa mlinzi na ukuta wa moto
kwa taifa hili. Hivyo Yerusalemu haitalindwa na ukuta wa mwanadamu bali na
ulinzi wa malaika wa Mungu.
Maneno
haya yawe kwetu maneno ya kutuhamasisha juu ya kuutumainia ulinzi wa Bwana.
Baadhi yetu tunalindwa na mbwa wakali, au silaha kali, au kampuni thabiti za
ulinzi na kukaa katika majengo yaliyowekewa uzio mkali wa umeme. Lakini
tusipokuwa makini katika kumtumainia Bwana, katika kumkaribisha Bwana alinde
kila tulichonacho, hakika hatuwezi kuwa salama. Tunakuwa salama kwa pale tu
Bwana anapokuja na kufanya makao katika miji na nyumba zetu. Kwani waweza kuwa
hata na ulinzi wa ukuta mkali lakini adui akaishia kutuvamia tu. Magonjwa mbalimbali
yanawasumbua hata walio katika ulinzi mkali. Haya hayawezi kukomeshwa kwa
silaha tulizo nazo au pesa zetu.
Tunahitaji
ulinzi wa Mungu. Shetani huzungukazunguka kama simba angurumaye akitafuta
mawindo. Hivyo yafaa tuwe imara. Tujifunze kumkaribisha Mwenyezi Mungu ili
achukue madaraka na ulinzi wa maisha yetu. Nguvu za mwanadamu hazitoshi.
Katika
somo la injili, Yesu anawaeleza wanafunzi wake ukweli wa mambo yatakayotukia
maishani mwake kwamba atateswa na kufa na siku ya tatu atafufuka. Lakini neno
hili linakuwa vigumu kupokelewa na wanafunzi wa Yesu. Na pia wanaogopa hata
kumuuliza. Haya yalitokea kwa sababu Yesu aliongea kuhusu ukweli wa maisha yake
jinsi ulivyo, uhalisia wa mambo yatakavyokuwa kwamba itambidi kuteswa. Lakini
inakuwa vigumu kwa uhalisia huu kupokelewa. Na ikiwa Yesu angeukataa uhalisia
huu, kwa hakika angalishindwa kutekeleza wajibu wake, na hata kutimiza lengo
liliomleta.
Sisi
tuwe watu wenye kukubali, wenye kukubali uhalisia wa maisha yetu. Tuzikubali
hali zetu, kama tunataka kweli kuwa wafuasi wa Bwana. Tusinganganie kile
wanachotaka wenzetu bali tutimize kile kinachotakiwa na uhalisia wa maisha
yetu. Tuishi sisi kama sisi, tuishi utume na majukumu ya Bwana.
------------------------
Copyright ©2013-2020
©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment