ASALI ITOKAYO MWABANI”
Tafakari ya kila siku
Alhamisi, Septemba 2, 2021
Juma la 22 la Mwaka wa
Kanisa
Sala ya Kanisa
(Zaburi)-Juma la 2
Kol 1: 9-14;
Zab 98: 2-6;
Lk 5: 1-11
NGUVU YA NENO LA YESU!
Karibuni sana wapendwa wa
Bwana kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo
la injili, tunakutana na Yesu akiingia katika mateso na shughuli za akina
Simoni. Anawakuta katika changamoto ya kupambana, wakivua samaki bila kupata
kitu. Yesu anawapatia maelekezo ya kufuata na hakika kwa njia ya yale
maelekezo, wanafaulu kwa kiasi kikubwa, kuliko hata walivyowahi kuona katika
historia yao ya uvuvi.
Wao walizoea kuvua usiku
kwani waliamini kwamba samaki hupatikana kwa wingi usiku kuliko mchana. Lakini
Yesu anawaeleza wavue mchana na kwa neno lake wanavua samaki wengi kuliko
walivyozoea kuvua usiku. Hakika neno la Bwana lina nguvu ajabu. Kwa neno lake
twaweza kufanya maajabu mengi. Neno hili litutie moyo kuanza shughuli zetu kwa
jina la Bwana. Tusianze chochote bila kulitaja jina la Bwana. Bila jina la
Bwana, tutavua usiku kucha bila kupata chochote kama ilivyotokea kwa akina
Petro.
Yesu katika injili,
anawaeleza akina Petro kwamba atawapa kazi mpya, kazi ya kuvua watu, kuwa
wavuvi wa watu na si samaki tena. Hii yamaanisha kwamba hakika Bwana Yesu
aliwapatia kazi yenye hadhi, kazi ya kuvua wanadamu. Sisi ndugu zangu, tumwombe
Bwana Yesu atupatie kazi yenye hadhi. Mara nyingi tunatumia muda wetu kwa
mizaha, kusengenya wengine na kutoa porojo nyingi. Bwana Yesu atatuonesha kazi
zenye hadhi-ambapo tutaweza kufungua macho na kuona mahitaji ya wenzetu, na
kuwasaidia. Sisi tuombe ili tuweze kufaidika kwa kazi za namna hii.
Katika somo la kwanza,
Paulo anawaombea wakristo wa Kolosai na kuwatakia matashi mema. Anasali kwa
ajili yao, wapate kumtambua Mwenyezi Mungu, watimize wajibu wao kwa Bwana na
kuzaa matunda mema kwa ajili ya kazi njema. Naomba sala na maneno haya ya Paulo
yatubariki na sisi. Tunahitaji kuombewa na kutakiwa matashi mema kama Paulo
anavyofanya. Nasi tuwe watu wa kuongea ujumbe wa matumaini kwa wenzetu kama
alivyofanya Paulo. Tuepuke kuwatukana wenzetu au kuwasema vibaya bali
tuwapelekee ujumbe wa matumaini kama anavyofanya Paulo leo.
------------------------
Copyright ©2013-2020
©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment