MASOMO YA MISA,
ALHAMISI, SEPTEMBA 2, 2021
JUMA LA 22 LA MWAKA
SOMO 1
Kol. 1:9-14
Tangu siku tuliposikia
habari yenu, hatuachi kufanya maombi na dua kwa ajili yenu, ili mjazwe maarifa
ya mapenzi yake katika hekima yote na ufahamu wa rohoni; mwenende kama ulivyo
wajibu wenu kwa Bwana, mkimpendeza kabisa; mkizaa matunda kwa kila kazi njema,
na kuzidi katika maarifa ya Mungu; mkiwezeshwa kwa uwezo wote, kwa kadiri ya
nguvu ya utukufu wake, mpate kuwa na saburi ya kila namna na uvumilivu pamoja
na furaha; mkimshukuru Baba, aliyewastahilisha kupokea sehemu ya urithi wa
watakatifu katika nuru.
Naye alituokoa katika
nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake;
ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi.
Neno la Bwana… Tumshukuru
Mungu.
________
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 98:2-6 (K) 2
(K) Bwana ameufunua
wokovu wake.
Bwana ameufunua wokovu
wake,
Machoni pa mataifa
ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa
nyumba ya Israeli. (K)
Miisho yote ya dunia
imeuona
Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi
yote,
Inueni sauti, imbeni kwa
furaha, imbeni zaburi. (K)
Mwimbieni Bwana zaburi
kwa kinubi,
Kwa kinubi na sauti ya
zaburi.
Kwa panda na sauti ya
baragumu.
Shangilieni mbele za
mfalme, Bwana. (K)
________
SHAGILIO
1Pet. 1:25
Aleluya, aleluya,
Neno la Bwana hudumu hata
milele, na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu.
Aleluya.
________
INJILI
Lk. 5:1 – 11
Makutano walipomsonga
Yesu wakilisikiliza neno la Mungu, yeye alikuwa amesimama kando ya ziwa la
Genesareti, akaona vyombo viwili vimekaa kando ya ziwa, lakini wavuvi wametoka,
wanaosha nyavu zao. Akaingia katika chombo kimoja, ndicho chake Simoni,
akamtaka akipeleke kidogo na pwani. Akaketi, akawafundisha makutano ali
chomboni.
Hata alipokwisha kunena,
alimwambia Simoni, Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki.
Simony akajibu akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku
kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu. Basi,
walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika;
wakawapungia mikono washirika wao waliokuwa katika chombo cha pili, waje
kuwasaidia; wakaja, wakavijaza vyombo vyote viwili, hata vikataka kuzama.
Simoni Petro alipona
hayo, alianguka magotini pa yesu, akisema, Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu
mwenye dhambi, Bwana. Maana alishikwa na ushangao, yeye na wote waliokuwa
pamoja naye, kwa sababu ya wingi wa samaki walaioupata; na kadhalika Yakobo na
Yohane, wana wa Zebedayo, waliokuwa washirika wa Simoni. Yesu akamwambia
Simoni, Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu. Hata walipokwisha kuviegesha
pwani vyombo vyao, wakaacha vyote wakamfuata.
Neno
la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 2020,
"MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment