“ASALI
ITOKAYO MWAMBANI”
Jumanne
, Septemba 21, 2021,
Juma
la 24 la Mwaka
Sikukuu
ya Mt. Mathayo, Mtume na Mwinjili
Efe
4:1-7, 11-13
Zab
19:1-4
Mt
9: 9-13
MUNGU
HAWAITI WAKAMILIFU,
ANAWAPA
UKAMILIFU WALE ALIO WAITA
Ndugu
wapendwa, karibuni kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana
katika asubuhi ya leo tunapoadhimisha sikukuu ya Mt. Mathayo tunakutana na
ujumbe maalumu toka katika somo la kwanza, Paulo anawaeleza Waefeso kwamba
wajitahidi kuwa waaminifu katika wito walioitiwa. Wanaelezwa wajione kama
sehemu ya mwili wa Kristo, yaani kanisa. Hivyo kama kiungo, kila mmoja
amekabidhiwa nafasi yake, kila mmoja anao umuhimu wao. Uzembe kidogo wa kiungo
kimoja utakosesha mwili wote nguvu.
Hivyo
siku zote wakristo wanapaswa kujiona kuwa wamoja, mwili mmoja wanaojenga kitu
kimoja chenye faida kwa wote. Ujumbe huu unamhamasisha kila Mkristo awe mtu wa
kujitahidi. Mt. Mathayo alitambua hili ndugu zangu, Mt. Mathayo baada ya
kutambua hili, alijitahidi sana kuishi nafasi yake kama kiungo muhimu cha
Kristo. Aliandika injili yake kwa kiebrania kwa lengo la kuwavuta Wayahudi
kwenye imani.
Sisi
tunapokumbuka Mt. Matayo, tuombe kutambua kwamba sisi ni sehemu ya mwili wa
Kristo, yaani kanisa. Hivyo tufanye yote kwa heshima ya Kristo na kanisa lake.
Tuondokane na kiburi au kufanya mambo yetu kibinafsi, ungana na kanisa katika
shughuli zako. Kabla ya kufanya uamuzi wetu wote, lazima tujitafiti na kuona
kwamba je, sisi kama wana wa kanisa, uamuzi huu utalisaidia vipi kanisa, au
utaliharibu vipi kanisa? Sisi ni viungo wake. Wengi wetu wanafanya maamuzi
mabovu baada ya kusahau kwamba wao ni wana wa kanisa. Kama wana wa kanisa,
hatupaswi kutembea wenyewe, tunapaswa kutembea na kanisa.
Liruhusu
kanisa liwe rafiki kwako.
Katika
injili, Yesu anamwita Matayo kuwa mtume wake. Anamkuta katika ofisi ya mtoza
ushuru na hapo anamwita katika kazi yake hiyo. Yesu anapofanya tukio hili
anapata marafiki watoza ushuru wengi. Yesu anasema waziwazi kwamba hakuja
kuwaita wenye haki bali wadhambi wapate kutubu.
Huyu
Matayo mtoza ushuru anapoitwa, na kuguswa na Yesu kwa namna ya pekee, anakuwa
tayari kuacha kazi yake, japo ya faida kwake kidunia na kumfuata Yesu. Hili
tukio liwe somo kwetu. Wengi wetu tupo kama huyu Matayo kwani bado tuna tozo za
ziada, tozo za zaidi tunazowafanyia wenzetu, ujira wa ziada, dhuluma
tunaowafanyia wenzetu na Yesu anakuja kwetu kila siku kwa namna ya pekee
akitutaka tuache tozo hiyo na kumfuata. Lakini wengi wetu tunafurahia hiyo
tozo, tunafurahia hiyo dhambi na kuona kwamba kwa sababu tunaendelea kufaidi,
kuishi maisha mazuri kutokana na hiyo dhuluma yetu au tozo ya ziada, hatupo
tayari kuacha.
Maisha
ya namna hii, yatatuangusha ndugu zangu. Tuwe hodari kama Matayo. Alikuwa
tayari kuacha kile kilichokuwa kinampatia raha, kafaida cha kidunia. Nawe
usione haya kukaacha. Hako ndicho kanachokuangusha. Kisikufanye wewe uchelewe
kufanya maamuzi. Unapaswa kufanya maamuzi sasa. Acha hako katabia.
------------------------
Copyright ©2013-2020
©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment