“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Jumanne Septemba 14,
2021.
Juma la 24 la Mwaka
Sikukuu ya Kutukuka kwa
Msalaba Mtakatifu
Hes 21: 4-9
Zab 77: 1-2, 34-38
Fil 2: 6-11
Yn 3: 13-17
MSALABA WA KRISTO NI
TUMAINI NA UKOMBOZI WETU!
Karibuni ndugu zangu kwa
adhimisho la Misa Takatifu. Ndugu zangu, leo tunaadhimisha sikuuu ya kutukuka
kwa msalaba. Masomo yetu ya leo yanatuongoza vyema kwenye kutafakari sikukuu
hii. Somo la kwanza linatoka katika kitabu cha Hesabu. Hapa tunawakuta wana wa
Israeli wanakosa Imani na kuanza kulalamika wakitaka kurudi Misri, wakale
matango, matikiti maji, na mboga. Mungu anakasirika na kupeleka nyoka wa sumu
wanao wauma na watu wengi kufa.
Wanamlilia Mungu naye
Musa anapewa njia ya ajabu kidogo ya kuwaokoa-ajabu kabisa-kutengeneza nyoka wa
shaba na kumwinua juu ya kamlingoti fulani halafu atakayemwangalia atapona tu,
ataokoka tu. Kwa kweli hii ilikuwa ni njia yakipekee kidogo-lakini Mungu
anaitumia.
Injili Yesu anapozungumza
na Nikodemus, tunapata maelezo ya kwa nini Mungu alitumia hii njia ambayo ni ya
pekee-lengo lilikuwa kutabiri wokovu. Alitabiri juu ya Mwanae atakayetundikwa
hivyo hivyo na kila atakayemwangalia, ataokoka tu.
Ulimwengu nyakati za Yesu
ulikuwa kama hili jangwa la Sinai. Watu walikuwa wamekosa Imani, wanamlalamikia
Mungu, wamechoka neema za Mungu-yaani chakula cha mbinguni-sasa wamesharudi
Misri kula yale matango, matikiti maji, vitunguu-ambayo ni kama mataputapu
tu-vitu kama ulevi, uasherati-ulafi, uonevu, majigambo-yote hayo ni matango
yaliyoko Misri-umeshachoka kula ile mana-yaani sakramenti-unataka ukale
matango-mataputapu, dhambi na ndiyo maana waliadhibiwa, watu walikuwa
wameshaanza kufa kwa dhambi kama wana wa Israeli walivyokufa kwa kungatwa na
nyoka.
Ulimwengu ukiwa katika
mataputapu hayo, Mungu anamtuma Mwana wake anakufa msalabani na kila
atakayemwangalia akiwa pale msalabani, ataokoka, ataponywa na sumu aliyopokea
kutokana na kutamani au kula hayo matango au matikiti maji yake aliyokwenda kuhangaikia.
Hivyo sikukuu ya leo ni
siku ya kumwangalia Yesu msalabani ili atuokoe na dhambi zetu. Ni siku ya
kuhakikisha kwamba tunatumia vizuri zile sakramenti alizozitoa kwa ajili yetu
wasafiri wa Jangwa la dunia. Usizichoke, usitamani matango kuliko mana na
kuanza kulalamika ati Mkate ule ule kila siku, mbona hata hatubadilishiwi uwe
na ladha fulani au na sukari-tupewe mkate mbadala bwana. Hapana! tusifanye
hivyo, hapa Mungu ataamka na hasira na kutumaliza.
Sisi tuwe watu wa
kushukuru. Tutumie vizuri sakramenti hizi alizotupa-watu hawazitaki kwa sababu
hazivutii-lakini kumbuka Waisraeli walisema hivyohivyo juu ya mana wakiwa
jangwani-wakidai imepoteza utamu-sisi tutumie sakramenti zote-na ndoa tufunge,
na kitubio tufanye, Ekaristi tupokee-na wale vijana ambao hatujapokea kipaimara
tupokee. Tusipozitumia sakramenti, nyoka wa sumu watatumaliza hapa
jangwani-duniani.
Hivyo basi msalaba ndio
nyoka yetu ile ya shaba. Tuutazame tupate kuponywa na nyoka waliotungata huku
ulimwenguni. Kila mmoja amekwishangatwa na nyoka huku ulimwenguni kutokana na
kiburi chake mbele ya Mungu. Wachunguze ni nyoka wapi wanaokungata na moja kwa
moja nenda mbele ya msalaba nawe utapona. Tusipokwenda hakika hatupo salama.
Pia ni lazima nasi
tukubali kuwa kama nyoka wa shaba kwa wengine, tuwe kama ishara ya msalaba kwa
wengine. Kila anayekutazama, atoke na tumaini, aponywe na nyoka wanaomngata.
Toa matumaini.
------------------------
Copyright ©2013-2020
©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment