Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

KUNGUTA MAVUMBI: NAKUACHA MAMBO YA ZAMANI

 

“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”

Tafakari ya kila siku

Jumatano, Septemba 22, 2021.

Juma la 25 la Mwaka

 

 

Ezra: 9: 5-9;

Tob 13: 2,4,6-8;

Lk 9: 1-6

 

 

KUNGUTA MAVUMBI: NAKUACHA MAMBO YA ZAMANI

 

Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Tafakari ya neno la Bwana katika somo la kwanza, Ezra anatoa sala ya kuukiri wema wa Mungu aliowatendea wana wa Israeli licha ya makosa yao. Aliwatendea wema bila ya wao kustahili kwani walikuwa wametenda dhambi. Ezra anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwahurumia, na kuwawezesha kutoka utumwani na kuweza kupata hekalu tena kwani kwa muda mrefu walikuwa bila hekalu, walikosa mahali pa kusali na kutoa dhabihu. Lakini sasa wemebarikiwa kwa kuweza kupapata mahali hapo na hivyo wanamshukuru Mungu kwa kuwatendea hili.

 

Na pia anatambua kwamba wao wamepatiwa ukombozi na kurudi katika nchi ya ahadi ili wamtumikie Mungu, ili waifanye kazi ya Bwana, ili watengeneze makao ya Bwana.

 

Ujumbe huu utufariji na sisi pia ndugu zangu. Tutambue kwamba Mwenyezi Mungu anapotupatia ukombozi, ni ili tuifanye kazi ya yake. Hatupatii ukombozi ili tukatukane watu, au tukajivune, au kudharau wenzetu au kutumia kwa anasa na kwa ulafi. Mwenyezi Mungu akitukomboa katika umaskini anafanya hivi ili wenzetu nao watumikiwe. Tujifunze kutoa kwa ajili ya kuwatumikia wenzetu na si kwa ajili ya kuwatesa au kunyanyasa.

 

Tusitumie kipaji, elimu, ujuzi au mali yetu kuinyanyasa jamii. Yote tunayopewa na Bwana yatumike kwa ajili ya Bwana.

 

Katika somo la injili, Bwana Yesu anatoa mamlaka kwa wanafunzi wake ya kwenda kuutangaza ufalme wa Mungu. Ufalme huu wahusu kuwaletea wenzetu matumaini na kuwaganga jeraha zao. Sisi tutambue kwamba kila mfuasi wa Kristo amepewa mamlaka haya. Hivyo tutumike katika kuutangaza ufalme wa mbinguni. Tunao uwezo: tuna vipaji mbalimbali, tunao muda mwingi pia, tunao ulimi wa kuwafariji wenzetu na masikio ya kusikia shida za wenzetu na pia macho ya kuona shida za wenzetu.

 

Hivyo tutumie nyenzo hizi kuona kweli ufalme huo wa Mungu na kuutangaza. Tuepuke tabia za hasira na kukunguta mavumbi kwa haraka na kuwa watu wa laana. Lazima tusiwe wepesi wa kukunguta mavumbi kama ishara ya kuwalaani wenzetu. Tumeumbwa ili tuvumilie na hivyo kila mmoja wetu avumilie kweli.

 

------------------------

Copyright ©2013-2020 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment