Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

KUKUWA KIUNDANI ZAIDI NDANI YA KRISTO!

 

“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”

Tafakari ya kila siku

Alhamisi, Septemba 23, 2021.

Juma la 25 la Mwaka

 

Hag 1: 1-8;

Zab 149:1-6, 9;

Lk 9: 7-9

 

 

KUKUWA KIUNDANI ZAIDI NDANI YA KRISTO!

 

Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo la kwanza Nabii Hagai ananyanyuka kuwahimiza watu wajenge hekalu la Bwana. Hiki ni kizazi ambacho wazazi wao walikuwa uhamishoni, sasa wamerudi tena katika nchi ya Yuda na kuanza kupata maisha bora. Walitumia rasilimali za nchi ile wakajenga majumba yao makubwa, na kumbi za starehe na za biashara. Lakini cha ajabu ni kwamba hakuna aliyehangaika na hekalu la Bwana.

 

Watu walikuwa wakiridhika kwenda kusali kwenye hekalu lilolo gofu, lililobomoka, linalovuja. Hagai anawahimiza waijenge nyumba ya Bwana. Wasifikirie kwamba wakitoa kwa ajili ya Bwana watakuwa maskini. Badala yake watambue ubaya uliopo katika kuhifadhi ya dunia, kuweka moyo wao kwa ya dunia kwa kuvaa nguo, kwa kuhangaikia chakula, na majengo. Watanunua na kuvaa nguo labda wakitegemea wapendeze lakini muda sio mrefu watajiona kwamba hawapendezi tena kwani nguo hutoka na fashion. Baada ya mwaka fashion hiyo hupita na unapoivaa hupendezi tena.

 

Hata vitu kama simu fashion yao hupita. Kwa sasa yaweza kuonekana kuwa nzuri naya kisasa lakini baada ya mwaka fashion inapitwa na wakati. Hata vitu kama majengo, kwa sasa yataonekana kuwa mazuri lakini baada ya muda yataonekana kupungua kwa uzuri wake pia. Hivyo wanachoweza kujivunia ni kumtumikia Bwana. Hivyo watoe vitu vyao kwa ajili ya Bwana.

 

Ujumbe huu ututie moyo hasa kwa baadhi yetu tusiojali sehemu zetu za ibaada. Wapo baadhi tunaoridhika kukalia mkeka kila tujapo kanisani au sehemu ya ibaada lakini nyumbani mwetu tunakalia vitu vyema. Wapo tunaovaa mavazi mazuri, tunavaa tai na nguo nzuri na kumbe tunasali kwenye kigango kisichokuwa na bati. Lazima tubadilike na kulipenda kanisa, nyumba yetu ya ibada. Usiridhike nguo za Padre zimechakaa na wewe unabadilisha suti kila siku, mtazame kuhani wako pia, anakula nini, wanapolala, nyumba yao ipoje?

 

Katika somo la injili, Herode anapata mshtuko kutokana na yote yanayotendwa na Yesu. Herode anaishi kwa wasiwasi kwa sababu ya dhambi yake aliyoitenda ya kumwua Yohane. Nasi tuogope ubaya wa dhambi. Hakika tutaitenda sasa lakini itatufanya tubabaike kwa mwaka mzima.

 

Tujifunze kuomba msamaha kwa pale tutendapo dhambi kwani tukiishi na dhambi bila kuomba msamaha, ni mzigo kwa maisha yetu, ni mzigo kwa nafsi zetu na wale wanaotutunza. Tujitahidi kuishi kwa ajili ya Bwana na kupenda mema.

------------------------

Copyright ©2013-2020 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment