“ASALI
ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari
ya Kila siku
Jumanne,
Septemba 28, 2021,
Juma
la 26 la Mwaka
Zek
8: 20-23;
Zab
86: 1-7;
Lk
9: 51-56
KUKABILIANA
NA KUKATALIWA!
Karibuni
sana wapendwa wa Bwana kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la
Bwana leo katika somo la injili ambapo Yesu anakataliwa na Wasamaria. Yesu
alipokuwa anakwenda huku Samaria, alikuwa haendi kuomba kwao bali alitaka
kuwahuburia ufalme wa mbinguni. Wao ndio wangalifaulu, magonjwa yao
yangaliponywa na kuishi kwa amani zaidi. Lakini wanatokea wachache wanaopinga
hili na kumfanya Yesu ashindwe kufanya utume huu.
Wanafunzi
wake wanamshauri ashushe moto lakini Yeye anakataa kutumia mamlaka haya. uamuzi
alioufanya Yesu unakuwa fundisho kwetu. Yesu alikuwa na mamlaka lakini anakataa
kuyatumia kwani alitambua kwamba yeye hakuja ili watu walaaniwe bali watu
wapate baraka. Yesu alikuja kuvunja vichaka vya fujo, na chuki na laana na
hivyo alijiepusha sana na kulaani yeyote.
Nasi
ndugu zangu tuwe na moyo wa kubariki wenzetu. Tusipende kulaani, tumetumwa ili
tuvunje laana, usipende watu waumwe, wafe au wapate ajali. Mtu anayelaani ni
mtu mwenye chuki, na pia kulaani laani ni dalili ya kuishiwa pesa. Watu
wanapoanza kufilisika ndio wanaanza kulaani. Tuepuke na tabia za namna hii,
tusipende kufurahia misiba ya wenzetu, au maumivu au matatizo ya wenzetu.
Katika
somo la kwanza, Zekaria anazidi kumweleza Israeli juu ya faida iliyopo pale
Bwana atakapokuja kati yao. Ni kwamba watakuwa na hekima, na watu watatoka
mbali ili kupata hekima hii kwao. Hii ni kwa sababu kumcha Bwana ni msingi wa
hekima. Moyo wa mwanadamu hauwezi kutulizwa na maneno ya hekima au elimu ya
kibinadamu. Mt. Augustino anasema kwamba mioyo yetu haitatulia hadi
itakapotulia katika wewe ee Bwana.
Sisi
tunapaswa kusali, kusafisha uovu wetu, tupate kuwa watu wenye hekima zaidi ili
basi wenzetu wapate kutulizwa na maneno na matendo yetu. Tusiposali kabla ya
kumshauri mwezetu maneno yetu hubadilika na kuwa umbea. Tujitahidi kupambana na
maneno yetu ya kimbea kwa njia ya kusali. Tumsifu Yesu Kristo.
------------------------
Copyright ©2013-2020
©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment