MASOMO YA MISA,
ALHAMISI, AGOSTI 19, 2021,
JUMA LA 20 LA MWAKA
INJILI
Mt. 22:1 – 14
Yesu aliwaambia makuhani
na makutano kwa mithali, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja
aliyemfanyia mwanawe arusi. Akawatuma watumwa waake wawaite walioalikwa kuja
arusini; nao wakakataa kuja. Akatuma tena watumwa wengine, akisema, Waambieni
wale walioalikwa, Tazameni, nimeandaa karamu yangu, ng’ombe zangu na vinono
vimekwisha kuchinjwa, na vyote vimekuwa tayari, njoni arusi. Lakini hawakujali,
wakaenda zao, mmoja shambani kwake, mmoja kwenye biashara yake; nao waliosalia
wakawakamata watumwa wake, wakawatenda jeuri, na kuwaua. Basi yule mfalme
akaghadhibika; akapeleka majeshi yake, akawaangamiza wauaji wale, akauteketeza
mji wao.
Kisha akawaambia watumwa
wake, Arusi i tayari, lakin wale walioalikwa hawakustahili. Basi enendeni hata
njia panda za barabara, na wote mwaonao waiteni arusini. Watumwa wale wakatoka
wakaenda njia kuu, wakakusanya wote waliowaona, waovu kwa wema; arusi ikajaa
wageni.
Lakini alipoingia yule
mfalme ili kuwatazama wageni wake, akaona mle mtu mmoja asiyevaa vazi la arusi.
Akamwambia, Rafiki, uliingiaje humu nawe huna vazi la arusi? Naye akatekewa.
Mfalme akawaambia watumishi, Mfungeni mikono na miguu, mchukueni mkamtupe
katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Kwa maana waitwao ni
wengi, bali wateule ni wachache.
Neno la Bwana...Sifa
kwako, ee Kristo
Copyright © 2020,
"MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment