MASOMO YA MISA, AGOSTI 14,
2021
JUMAMOSI, JUMA LA 19 LA
MWAKA
SOMO 1
Yos. 24:14-29
Yoshua aliwaambia
makutano: Sasa mcheni Bwana, mkimtumikia kwa unyofu wa moyo na kwa kweli; na
kuiweka mbali miungu ambayo baba zenu waliitumikia ng’ambo ya Mto, na huko
Misri; mkamtumikie yeye Bwana. Nanyi kama mkiona ni vibaya kumtumikia Bwana,
chagueni hivi leo mtakayemtumikia; kwamba ni miungu ile ambayo baba zenu
waliitumikia ng’ambo ya Mto, au kwamba ni miungu ya wale Waamori ambao mnakaa
katika nchi yao; lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia Bwana.
Hao watu wakajibu
wakasema, Hasha! Tusimwache Bwana, ili kuitumikia miungu mingine; kwa maana
Bwana, Mungu wetu, yeye ndiye aliyetupandisha sisi na baba zetu kutoka nchi ya
Misri; kutoka nyumba ya utumwa; naye ndiye aliyezifanya ishara zile kubwa mbele
ya macho yetu, na kutulinda katika njia ile yote tuliyoiendea, na kati ya watu
wa mataifa yote tuliopita katikati yao. Bwana ndiye aliyewafukuza watu wa
mataifa yote watoke mbele yetu, naam, Waamori waliokaa katika nchi hii; basi,
kwa ksababu hiyo sisi nasi tutamtumikia Bwana; maana yeye ndiye Mungu wetu.
Yoshua akawaambia watu,
Hamwezi kumtumikia Bwana; kwa kuwa yeye ni Mungu mtakatifu; yeye ni Mungu
mwenye wivu; hatawasamehe makosa yenu, wala dhambi zenu. Kama mkimwacha Bwana
na kuitumikia miungu migeni, ndipo atageuka na kuwatenda mabaya na
kuwaangamiza, baada ya kuwatendea mema.
Lakini hao watu
wakamwambia Yoshua, La! Lakini tutamtumikia bWana. Yoshua akawaambia watu,
Ninyi mmekuwa mashahidi juu ya nafsi zenu, ya kuwa mmemchagua Bwana, ili
kumtumikia yeye. Wakasema, Sisi tu mashahidi. Akasema, Basi sasa, iondoeni
miungu migeni iliyo kati yenu, mkaielekeze mioyo yenu kwa Bwana, Mungu wa
Israeli. Ndipo hao watu wakamwambia Yoshua, Bwana, Mungu wetu, ndiye
tutakayemtumikia; na sauti yake ndiyo tutakayoitii.
Basi Yoshua akafanya
agano na wale watu siku ile, akawapa amri na agizo huko Shekemu. Yoshua
akayaandika maneno haya katika kitabu cha torati ya Mungu; kisha akatwaa jiwe
kubwa, akalisimamisha huko, chini ya ule mwaloni uliokuwa karibu na patakatifu
pa Bwana.
Yoshua akawaambia watu
wote, Tazama, jiwe hili litakuwa shahidi juu yetu; kwa maana limesikia maneno
yote ya Bwana aliyotuambia, basi litakuwa shahidi juu yenu, msije mkamkana
Mungu wenu. Basi Yoshua akawaruhusu watu, wakaenda zao, kila mtu kwenye urithi wake.
Ikawa, baada ya hayo,
Yoshua, mwana wa Nuni, mtumishi wa Bwana, akafa, mwenye umri wa miaka mia na
kumi.
Neno la Bwana...
Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 16:1-2, 5, 7-8, 11
(K) 5
(K) Bwana ndiye fungu la
posho langu.
Mungu unihifadhi mimi,
Kwa maana nakukimbilia
Wewe.
Nimemwambia Bwana, Ndiwe
Bwana wangu;
Sina wema ila utokao
kwako. (K)
Bwana ndiye fungu la
posho langu,
Na la kikombe changu;
Wewe unaishika kura
yangu.
Nitamhimidi Bwana
aliyenipa shauri,
Naam, mtima wangu
umenifundisha usiku. (K)
Nimemweka Bwana mbele
yangu daima,
Kwa kuwa yako kuumeni
kwangu, sitaondoshwa.
Utanijulisha njia ya
uzima;
Mbele za uso wako ziko
furaha tele;
Na katika mkono wako wa
kuume
Mna mema ya milele. (K)
SHANGILIO
Yak. 1:18
Aleluya, aleluya,
Kwa kupenda kwake
mwenyewe, Baba alituzaa sisi kwa neno la kweli, tuwe kama limbuko la viumbe
vyake.
Aleluya.
INJILI
Mt. 19:13 – 15
Yesu aliletewa watoto
wadogo ili aweke mikono yake juu yao na kuwaombea; wanafunzi wake wakawakemea.
Lakini Yesu akasema, Waacheni watoto wadogo waje kwangu; wala msiwazuie; kwa
maana walio mfano wa hao, ufalme wa mbinguni ni wao. Akaweka mikono yake juu
yao, akatoka huko.
Neno la Bwana... Sifa
kwako Ee Kristo.
Copyright © 2020,
"MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment