“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Jumamosi, Agosti 14 2021
Juma la 19 la Mwaka
Kumbukumbu ya Bikira
Maria
_____________________________
Yos 24: 14-29;
Zab 15: 1-2, 5, 7-8, 11;
Mt 19:13-15
___________________
KUMPOKEA YESU KAMA
WATOTO!
Ndugu zangu wapendwa,
karibuni kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana, katika
somo la kwanza, Yoshua anawaeleza wana wa Israeli kwamba yeye na familia yake
watamtumikia Bwana. Kwa nini Yoshua aseme yote haya? ni kwa sababu kipindi hiki
wapo katika nchi ya ahadi, na hapa wanafurahia maisha, hawapo tena katika
jangwa.
Kilichotokea ni kwamba
kuna kizazi kilichozaliwa katika nchi ya ahadi ambacho hakikuyaona maajabu ya
Mungu tangu walipokuwa Misri. Wala hakikujua kwamba baba zao walipata shida
jangwani na kusaidiwa kwa nguvu ya mkono wa Mungu. Wao walianza kuambatana na
baadhi ya makabila ambayo hata hapo mwanzoni yalikuwa maadui yao, makabila
ambayo yalikuwa hayataki wana wa Israeli waingie hata katika nchi ya ahadi.
Walianza kukumbatia tamaduni zao, na kuoa na kukubali kuolewa nao. Joshua
anatoa onyo kwa watu wa namna hii.
Anawaeleza kwamba ulizeni
historia yenu, ulizeni jinsi mlivyowahi kusaidiwa na Bwana. Hivyo msimwache
Bwana Mungu wenu.
Ujumbe huu utusaidie na
sisi pia. Tuwe watu wa kuulizia historia zetu. Wapo baadhi yetu ambao
tumezaliwa na kukuta wazazi wetu wametuandalia mambo mazuri, lazima tuwe tayari
kuuliza haya mambo mazuri yalianzaanzaje, tusianze kutumia tu bila
kujikumbushia historia ya vitu unavyotumia. Wapo pia ambao wameolewa na kukuta
mambo mazuri, lazima tuwe tayari kuuliza huyu mtu alianzaanzaje akafikia hapa?
Usianze kutumia bila kuulizia historia. Historia itakufanya mnyenyekevu na
kumkumbuka Bwana Mungu wetu; kwa sababu wengi wetu historia zetu ni dhaifu na
zenye kutunyenyekesha.
Katika somo la injili,
Yesu anasema kwamba ufalme wa mbinguni ni kwa ajili ya wale walio kama watoto.
Watoto ni wanyenyekevu na wenye matumaini makubwa. Huwa wakifundishwa-wanaamini
haraka. Sio wepesi wa kupinga ujumbe au fundisho hasa wakijua kwamba latoka kwa
wazazi wao au watu wao wa karibu. Mungu ndiye mtu wetu wa karibu. Lazima tuwe
tayari kupokea maagizo yake na mafundisho yake kama watoto wadogo. Hii ndiyo
imani, hapa ndipo kujijengea baraka, hapa ndipo kuwa mkubwa katika ufalme wa
mbinguni.
------------------------
Copyright ©2013-2020
©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment