“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Jumatano, Agosti 18, 2021
Juma la 20 la Mwaka
___________________
Amu 9: 6-15;
Zab 20: 2-7;
Mt 20:1-16
___________________
JE, UNAKUWA NA WIVU
MWENZAKO ANAPO FANIKIWA?
Karibuni sana ndugu zangu
wapendwa kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana katika
somo la kwanza tunakutana na wana wa Israeli wakiwa katika nchi ya ahadi;
hakika wanashindwa kuifurahia nchi hii. Kile walichoahidiwa hawakioni kwa
sababu wameyakiuka maongozi ya Mungu. Wanaishi kwa kuyaiga mataifa mengine
yaliyowazunguka. Wao walifikiria kwamba mataifa mengine yalifurahia kwa sababu
wao walikuwa na mfalme.
Kitendo cha wao kukosa
mfalme wa kibinadamu kama hayo mataifa mengine kiliwafanya wajifikirie kwamba
ndio sababu za wao kushindwa kuishi maisha ya raha. Na leo wanajichagulia
mfalme aliyeitwa Abimeleki. Na huyu mfalme kwa hakika alileta shida badala ya
raha kwa wana wa Israeli. Huyu mfalme atawaletea moto badala ya kuwapa utulivu.
Ndugu zangu, haya ndio
matokeo ya kuzitegemea nguvu zetu na kuacha kumtegemea Mwenyezi Mungu. Kile
tunachokichagua, tunachokiona kuwa chema kumbe tunakikuta kuwa hatari kubwa,
yenye kuiletea maisha yetu maangamizi kama Abimeleki alivyokuwa kwa wana wa
Israeli. Hivyo tuache kuzitegemea nguvu zetu zaidi kuliko kumtanguliza Mwenyezi
Mungu mbele.
Wengi wetu tumeanguka kwa
sababu ya kujiamini kupita kiasi. Tukumbuke udhaifu wetu na kuwa wapole na
wenye hekima zaidi.
Katika somo la injili,
Yesu anatoa mfano wa wafanyakazi waliokwenda katika shamba la mizabibu na
kulipwa mshahara mmoja. Yawezekana wale waliofika mara ya mwisho walionesha nia
ya kufanya kazi kwa bidii zaidi na ndani ya muda mfupi, nia yao iliweza
kumfurahisha mwajiri kuliko walivyokuwa wale wa kwanza. Wale wa mwisho hakika
walikuwa na nia ya kufanya kazi kwani walikuwa tayari kukaa sehemu ya soko hadi
jioni wakiwa wakitafuta kazi. Hivyo mwajiri alifurahishwa sana na nia na
utayari wa hawa waliokuwa tayari kufanya kazi.
Hakika Mwenyezi Mungu
naye huangalia nia na utayari. Utayari wa namna hii na bidii ndio utakaotufanya
tuingie mbinguni. Hivyo tuwe na nia na bidii na utayari wa kufanya kazi katika
shamba la Bwana. Shamba la Bwana lina wafanyakazi wengi lakini wengi wetu
hatuna nia ya kufanya kazi. Tuwe na nia ya kufanya kazi kama wale wafanyakazi
ambao walikuwa tayari hadi mwisho. Tumsifu Yesu Kristo.
------------------------
Copyright ©2013-2020
©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment