“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya Kila siku
Jumamosi, 24 Julai, 2021,
Juma la 16 la Mwaka
Kut 24:3-8;
Zab 34:1-10
Yn 11:19-27
Uwe urithi wetu.
Karibuni sana wapendwa
wangu kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Leo tunaadhimisha
kumbukumbu ya Wat. Yoakimu na Anna, Wazazi wa Mama Bikira Maria. Wazazi hawa
wanaheshimika kwa sababu wamekuwa sababu ya mtoto wao, Maria, aliyekuja kuwa
Mama wa Mkombozi wetu Yesu Kristo.
Wazazi hawa walijitahidi
kumtunza mpendwa wa Mungu, mnadhiri wa Mungu na hakika akafanikiwa kuja kuwa
mama wa Mkombozi wetu Yesu Kristo. Ni somo na fundisho kwetu, kuwatunza
wapendwa wa Bwana. Wale wanaoonesha nia ya kumtumikia Mungu, yafaa tuwatie
moyo, tuwapatie mazingira bora, tuwaepushe na mazingira yaliyojaa maneno
machafu. Tuepuke kuwakwaza wale wanaopenda kumtumikia Mwenyezi Mungu kama
alivyofanya Mama Maria. Mapokea yanatueleza kwamba wazazi hawa walimpeleka
mtoto wao, yaani Maria katika hekalu na huko alianza kujifunza maisha ya
kumtumikia Mungu tangu utoto wake. Hii ilikuwa hazina kubwa kwake kwani
ilimfanikisha sana maishani na kuishi maisha ya amani.
Sisi kama wazazi tutambue
kwamba miongoni mwa zawadi kuu tuwezazo kuwapatia watoto wetu na vijana wetu ni
zawadi ya kumpenda Mungu. Ukiona kijana au binti yako anampenda Mungu, hapa
ndio unaweza kusema kwamba umefaulu. Kwa sababu asiyejali, asiyemjua Mungu
huwezi kumtegemea kwa lolote. Anaweza kuwa na uwezo kifedha lakini haaminiki au
huwezi kumtegemea kwa lolote. Lakini kama anamfahamu Mungu, na anajali, hii
ndio zawadi kubwa tuwezayo kumwachia. Na kwamba unamuacha mtu ambaye
anaaminika, anaweza kutekeleza kazi, na kuwa mwanga kwa wenzao.
Sisi tujifunze kuwaachia
watoto wetu urithi wa kumcha Mungu. Uwe urithi wetu.
Katika somo la injili,
Yesu anawaeleza wanafunzi wake kwamba heri macho yao kwa kuwa yanaona na
kusikia yale wanayoyasikia sasa. Wapo wengi waliotamani kukutana na Yesu na
kumuona akifanya kazi ya umasiha. Yesu alizaliwa na Bikira Maria na Maria
alikuwa mtoto wa Yoakimu na Anna. Hivyo Yesu alikuwa sababu ya Mama Maria,
pamoja na Yoakimu na Anna kupata sifa kuu. Sisi tutambue kwamba maadili yetu
mema na maisha yetu yenye adili yatawafanya wazazi wetu na ndugu zetu wapate
sifa. Maisha yetu mabaya ni sababu ya wazazi wetu na pia ndugu zetu kupata sifa
mbaya na kuishi katika huzuni. Tuishi kimaadili kadiri ya Injili tunayosikia
sasa ili tuweze kuwa sababu ya furaha kwa vizazi vyetu.Tumsifu Yesu Kristo
------------------------
Copyright ©2013-2020
©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment