MASOMO YA MISA, JULAI 24, 2021
JUMAMOSI, JUMA LA 16 LA
MWAKA
SOMO 1
Kut. 24:3-8
Musa aliwambia watu
maneno yote ya Bwana, na hukumu zake zote; watu wote wakajibu kwa sauti moja,
wakasema, Maneno yote aliyoyanena Bwana tutayatenda. Basi Musa akayaandika
maneno yote ya Bwana, akaondoka asubuhi na mapema, akajenga madhabahu chini ya
mlima, na nguzo kumi na mbili, kwa hesabu ya kabila kumi na mbili za Israeli,
akapeleka vijana wa wana wa Israeli, waliotoa sadaka za kuteketezwa,
wakamchinjia Bwana sadaka za amani za ng’ombe.
Musa akatwaa nusu ya ile
damu, akaitia katika mabakuli; na nusu ya ile damu akainyunyiza juu ya
madhabahu. Kisha akakitwaa kitabu cha agano akakisoma masikioni mwa watu;
wakasema, Hayo yote aliyoyanena Bwana tutayatenda, nasi tutatii. Musa akaitwaa
ile damu, akawanyunyizia watu, akasema, Hii ndiyo damu ya agano alilolifanya
Bwana pamoja nanyi katika maneno haya yote.
Neno la Bwana...
Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 50:1-2, 5-6, 14-15
(K) 14
(K) Mtolee Mungu dhabihu
za kushukuru.
Mungu, Mungu Bwana,
amenena, ameiita nchi,
Toka maawio ya jua hata
machweo yake.
Tokea Sayuni,, ukamilifu
wa uzuri,
Mungu amemulika. (K)
Nikusanyieni wacha Mungu
wangu,
Waliofanya agano nami kwa
dhabihu.
Na mbingu zitatangaza
haki yake,
Kwa maana Mungu ndiye
aliye hakimu. (K)
Mtolee Mungu dhabihu za
kushukuru;
Mtimizie Aliye juu
nadhiri zako.
Ukaniite siku ya mateso;
Nitakuokoa, na wewe utanitukuza.
(K)
SHANGILIO
Zab. 8:15
Aleluya, aleluya,
Wanabarikiwa wale ambao
kwa unyofu na wema wa mioyo yao, hulisikia neno la Mungu na kulishika.
Aleluya.
INJILI
Mt. 13:24 – 30
Yesu aliwatolea makutano
mfano akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema
katika konde lake; lakini watu walipolala akaja adui yake akapanda magugu
katikati ya agano, akaenda zake. Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa,
yakaonekana na magugu. Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda
mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu? Akawaambia, Adui
ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye?
Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing’oa ngano pamoja nayo. Viacheni
vyote vikue hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao,
Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano
ikusanyeni ghalani mwangu.
Neno la Bwana... Sifa
kwako Ee Kristo.
No comments:
Post a Comment