"ASALI ITOKAYO
MWAMBANI"
Tafakari ya kila siku
Jumamosi, Julai 10, 2021
Juma la 14 la Mwaka
Kumbukumbu ya Mtakatifu
Bonaventure, Askofu na Mwalimu wa Kanisa
Mwa 49: 29-33, 50:15-25;
Zab 105: 1-4, 6-7 (R) Ps.
69:32;
Mt 10: 24-33.
MSIOGOPE
Ndugu zangu wapendwa,
karibuni kwa adhimisho la misa takatifu. Neno la Bwana katika somo la kwanza,
tunapewa habari juu ya kifo cha Yakobo na Yusufu. Wote hawa walikuwa watu wema
walioifuata njia ya Bwana. Yusufu anasifika kwa tabia yake ya kuwasamehe ndugu
zake kuepuka kuwatangazia kisasi ndugu zake. Jambo hili lilimfanya aendelee
kubarikiwa na Bwana. Lakini pia liliwaletea fundisho ndugu zake kwani kama
tunavyosikia katika somo la kwanza, wao walizidi kuhaha na kuwa na wasiwasi
wakifikiria kwamba Yusufu atawalipiza kisasi. Lakini cha ajabu Yusufu
hakutangaza adhabu.
Nasi tunaalikwa kumwiga
Yusufu. Tutambue kwamba pale tutakapoepuka roho ya kisasi hapa ndipo chanzo cha
sisi kubarikiwa zaidi. Na hapa tutaweza kutumika na Mungu kama vyombo vya
kuwafundishia wenzetu hasa wale waliotutendea uovu. Lakini kama tutakuwa watu
wa kurudisha visasi tutambue kwamba kwa hakika hatutaweza kutumika kama vyombo
vya kuwafundisha wenzetu na Bwana. Tukubali kuacha roho ya kisasi na hakika
tutaweza kuona baraka kubwa toka kwa Mwenyezi Mungu.
Katika somo la injili,
Yesu anawapatia wafuasi wake ujumbe wa matumaini kwamba hakika hawapaswi
kuogopa, wawe na tumaini kwa Mungu kwani hata nywele za vichwa vyao
zimehesabiwa tayari. Huu ulikuwa ujumbe wenye lengo la kuwatia matumaini kwamba
wasiogope mateso bali wamtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika tumaini lao
halitawahadaa, bali litawapatia uzima wa milele. Huu ndio upendo wa Mwenyezi
Mungu kwetu. Hakika anaona kila kilicho chetu, mateso yetu na maumivu yetu yote
anayaona. Sisi tuzidi kumtegemea Mwenyezi Mungu. Hakika atatuokoa na kutupatia
ukombozi.
Pia anajua kila kitu.
Hata kipindi cha mateso bado yupo nasi. Shetani ana lengo la kutuonesha kwamba
sisi tumeachwa pweke. Hivyo anataka yeye aingie na kututawala. Ndivyo shetani
alivyo. Lakini yafaa tutambue kwamba pale tunapojisikia kuwa wapweke sana ndio
Mungu yupo karibu zaidi. Shetani lengo lake ni kutufanya tujisikie huo upweke
na hofu ili basi tugeuke na kumfuata yeye. Tusikubali.
------------------------
Copyright ©2013-2020
©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment